Sababu zilizopelekea serikali kusitisha utoaji wa 'passport' za makundi

Serikali imesitisha utoaji wa pasi za kusafiria ‘passport’ za jumla za makundi mpaka pale utakapopatikana utaratibu rasmi na mzuri kati ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya nchi husika.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt Mwigulu Lameck Nchemba kufuatia kuwepo kwa mikasa ya kunyanyaswa, kutumikishwa na kuteswa kikatili  kwa baadhi ya watanzania wanaokwenda nje ya nchi kwa jili ya kufanya kazi mbalimbali ikiwemo kazi za ndani.

“Nimezipata taarifa hizo za mateso ya watu wetu wanaokwenda nje ya nchi kwa kazi tofauti tofauti…. Nasimamisha utoaji wa pasport za jumla za makundu ya vijana ambao wamekuwa wakikutana na mikasa hiyo ya kunyayaswa, kutumikishwa, kuteswa kikatili na wengine kuwekwa rehani kwa maswala ya dawa za kulevya. tunasimamisha mpaka pale tutakapokuwa tumeweka utaratibu ulio rasmi na utaratibu mzuri kati ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya nchi husika ambako kutakuwa na mahitaji ya namna hiyo,” amesema Waziri Dkt Nchemba.

Waziri Dkt Nchemba ameeleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa ili kuwanusuru vijana wa Tanzania kutokana na mateso na ukatili ikiwamo kuwekwa rehani kwa madawa ya kulevya pamoja na kunyang’anywa passport na kutumikishwa.

Vilevile Waziri Nchemba ameelza kuwa, kumekuwa na tabia ya watu kuingiza raia wa kigeni hapa nchini na wanapowaingiza wanawafanyisha shughuli nyingine ambazo ni tofauti na zilizopo kwenye vibali vyao, huku akiwataka wote wanaofanya hivyo kuripoti leo, na tofauti na hapo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Wako raia wanaoingia kwa makundi nchini kwetu, na wale wanaowaleta wanatumia sababu tofauti wanapowaleta, na wanapoingia wanawafanyisha shughuli tofauti na walizoombea vibali. Watu wote wanaoomba vibali na baadae wakatumia vibali hivyo tofauti ama wakafanya majukumu mengine tofauti na waliyoombea vibali, wanavunja sheria na watafika kwenye mkono wa sheria,” amesema Waziri Nchemba.

“Watu hawa naelekeza leo hihi hii waripoti kwa kamishna wa mipaka na Kamishna wa vibali… na kama mpaka jioni watakuwa hawajaripoti, wakamatwe na wafike kwenye mkono wa sheria, ili sheria iweze kufata mkondo wake,” ameongeza Waziri Nchemba.


from MPEKUZI

Comments