Mabilioni ya JPM zimebaki siku sita

Mabilioni  yaliyoahidiwa na Rais John Magufuli kwa wazabuni mbalimbali yanatarajiwa kuanza kutolewa kuanzia siku sita zijazo kama ilivyoahidiwa kutokana na zoezi la uhakiki kuwa kwenye hatua za mwisho.

Januari 3, mwaka huu, Rais Magufuli alisema angelipa madeni mbalimbali ya ndani yaliyohakikiwa ipasavyo kwa kutumia Sh. bilioni 200 zilizotengwa Februari.

"Uchumi unaenda vizuri sana, tuna pesa nyingi. Nimepanga kuanzia mwezi ujao (Februari), madeni ya ndani watu wanayodai; wazabuni waliosambaza chakula kwenye vyuo na shule, makandarasi na wafanyakazi kama walimu tutayalipa," alisema Rais Magufuli muda mfupi baada ya kukutana na Gavana mpya wa Benki Kuu, Florens Luoga Ikulu jijini Dar es Salaam.

"Yale madeni yote yatakayokuwa yamehakikiwa ilmradi yasiwe madeni hewa, mwezi unaokuja nitatoa bilioni 200 ziende zikalipe madeni," alisema.

Msemaji wa Wizara ya Fedha na Mipango, Ben Mwaipaja, jana alisema uhakiki unaendelea kufanyika maeneo mbalimbali, ili kujiridhisha na ukweli wa madeni hayo.

"Kwa sasa uhakiki unaendelea na kuanzia Februari agizo la Rais litatekelezwa kwa wale wote ambao wamehakikiwa na kujiridhisha na madeni yao tutaendelea kuwalipa kwa kuwa malipo ni endelevu," alifafanua Mwaipaja.

Rais Magufuli alipozungumza Ikulu alisema angeweza kutoa mapema fedha hizo, lakini ameona kuna umuhimu wa kuhakiki madeni husika na baada ya mchakato kukamilika ataruhusu zitolewe na kwenda kwa wananchi.

Aidha, Rais Magufuli alimwagiza Gavana Luoga kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango ili wadai wa serikali wa ndani waweze kulipwa kama njia ya kukuza uchumi kwa kuwa Sh. bilioni 200 zitasambaa kwa wananchi.

"Nina uhakika zitawasaidia wananchi ambao walikuwa waaminifu, waliokuwa wazabuni, nitahakikisha wenye madeni ya ukweli na siyo uongo kupata fedha za kuwasaidia kufanya biashara," alisisitiza Rais Magufuli.


from MPEKUZI

Comments