Masauni: Ni Aibu Kubwa Sana Madini Kutoroshwa Nchini na Kisha Kukamatwa na Nchi Jirani

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, amesema ni aibu kusikia nyara za Serikali ikiwamo madini zinatoroshwa na kukamatiwa nchi za jirani na kuagiza ulinzi wa kutosha katika viwanja vya ndege nchini.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku moja baada ya Rais Dk. John Magufuli kupokea dhahabu kutoka Kenya, ambayo ilitoroshwa nchini kupitia viwanja vya ndege vya Mwanza na Kilimanjaro na kukamatiwa Nairobi, Kenya.

Akipokea dhahabu hiyo juzi, Rais Magufuli alisifu vyombo vya ulinzi vya Kenya huku akieleza kusikitishwa na vya Tanzania kushindwa kukamata.

Masauni jana mara baada ya kukagua usalama wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam, alisema kupokea madini ya dhahabu kutoka Kenya kumemuhuzunisha yeye na Rais Magufuli.

Alisema jambo hilo halitavumiliwa kuendelea, ni lazima jitihada za makusudi zichukuliwe na ndiyo maana ameanza kukagua usalama wa viwanja huku akiwataka Mamlaka ya Mapato (TRA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) na Polisi wafanye kazi kwa pamoja.

“Hatua ya jana (juzi) ya Rais imeshtua sana na kuna haja ya kufanya kazi kwa muunganiko mkubwa kati ya Jeshi la Polisi, TRA, TAA ili kuhakikisha kunakuwa na usalama.

“Nimekagua kwa kuanza na huu uwanja mkubwa, nitaendelea katika viwanja vingine ili kuhakikisha naangalia maeneo ya usalama na hakuna mtu kupitisha dawa za kulevya, nyara za Serikali na vitu vingine visivyo halali,” alisema.

 Masauni alisema wataongeza kikosi cha askari wa kutosha na wenye sifa wenye mbwa kukagua mizigo na kubaini vitu ambavyo si halali ikiwemo dawa za kulevya.

Alisema ulinzi unatakiwa kuimarishwa, hasa kwa abiria wanaosafiri kwa kulinda mali zao, abiria wanaoingia nchini, mizigo na kuangalia usalama wa mali mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukamata wale wanaosafirisha dawa za kulevya na nyara za Serikali pia.


from MPEKUZI

Comments