Katibu Mkuu CCM Ammwagia Sifa Mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula....Atoa Onyo Kwa Wabunge Wazembe

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Dkt Bashiru Ally amesema hatashangaa kuona mbunge wa jimbo la Ilemela ambaye ni Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipita bila kupingwa katika uchaguzi mkuu ujao 2020 kutokana na kazi kubwa aliyoifanya ya kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo lake.

Dkt Bashiru alisema hayo tarehe 30 Julai 2019 katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza katika mkutano Mkuu wa Jimbo la Ilemela kuelezea utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi kama ilivyoahidiwa na Mbunge wa Jimbo hilo wakati wa kampeni za uchaguzi za mwaka 2015.

Katibu Mkuu huyo wa Chama cha Mapinduzi alisema hakuna kumnadi tena Dkt Angeline Mabula kwa kuwa anazo sifa zinazomuwezesha kutetea kiti chake na yeyote anayetaka kuwania nafasi katika jimbo hilo ajue kiti hicho kishakaliwa pamoja na kata zake 19.

Alionya Wabunge wa CCM waliozembea kufanya ziara za kutatua kero za wananchi  pamoja na kufanya vikao kwenye majimbo yao kuwa hawatakuwa na ulinzi wakati wa kinyanganyiro cha kupendekeza majina ya kuwania nafasi hizo na kusisitiza kuwa kipaumbele kitatolewa  kwa  wabunge waliokuwa wakichapa kazi.

Aliwaaambia wana Ilemela kuwa, kuna tofauti kubwa sana ya kimaendeleo wakati jimbo la Ilemela lilipokuwa chini ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na sasa linavyoshikiliwa na Chama cha Mapinduzi.


from MPEKUZI

Comments