Ajali Yaua Watano Mtwara Baada ya Gari Kupinduka na Kuwaka Moto

Watu watano wamefariki dunia baada ya gari aina ya Toyota Noah walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka, kisha kuwaka moto.

Akizungumza leo Alhamisi Juni 28, 2018 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Lucas Mkondya amesema ajali hiyo imetokea jana saa 10 jioni katika kijiji cha Chingweje wilaya ya Nanyumbu mkoani hapa.

Amesema kati ya waliopoteza maisha, wawili  wameungua na moto na  imeshindikana kuwatambua na wengine watatu wameungua kiasi, “kati ya waliofariki dunia ambao mpaka sasa wametambulika ni dereva wa gari hilo Babuu Maroro.”

Amesema  majeruhi wa ajali hiyo waliolazwa katika Hospitali ya Mkomaindo Masasi ni Daria Bushiri (30) mkazi wa Masuguru, Afkam Ling'ande (4) na Khalid Salum  ambaye ni kondakta wa gari hilo.

“Huyu Salum anashikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi maana aliruka kabla ya ajali kutokea. Eneo ilipotokea ajali kulikuwa na mteremko mkali na mbele zaidi kulikuwa na kosa, gari ilimshinda dereva na ikagonga gema la barabara na kupinduka, kuwaka moto,” amesema.

“Lilivyoanza kuwaka moto, watu watatu walitoka salama ila watano walioshindwa kutoka waliungua, kati yao wawili wameungua vibaya na hawatambuliki. Watatu kidogo wanaweza kutambulika. Tunaomba ndugu jamaa kujitokeza kutambua miili ya marehemu ambayo imehifadhiwa katika hospitali ya Mkomaindo.”


from MPEKUZI

Comments