Waziri wa Kilimo: Watakaoajiri Watoto Chini Ya Miaka 18 Kwenye Tumbaku Kukiona Cha Moto

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amesisitiza marufuku yake aliyoitoa hivi karibuni kuhusu ajira kwa watoto ambao wapo chini ya miaka 18.

Mhe Hasunga amepiga marufuku hiyo jana tarehe 30 Novemba 2019 wakati akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Kilimo Jijini Dar es salaam.

Alisema kuwa suala la ajira kwa watoto ni miongoni mwa mambo yanazuiliwa kwenye Sheria za kimataifa kupitia Shirika la Kazi Duniani (International Labour Organization) na Sheria za Ajira hapa nchini hivyo mdau yeyote atakayebainika kukiukwa maelekezo hayo atashtakiwa.

“Nawasihi wadau wote hususani wakulima wa Tumbaku tuendelee kupiga vita ajira kwa watoto kwa kuwa ni eneo ambalo limeendelea kulalamikiwa na wadau wengi” Alikaririwa Mhe Hasunga

Kadhalika, Mhe Hasunga alisema kuwa katika kuhakikisha zao la tumbaku linaendelea kutoa mchango mkubwa katika pato la mkulima na Taifa, Wizara imejiwekea malengo ya haraka yanayopaswa kutekelezwa ambayo ni pamoja na usajili wa wakulima wote wa tumbaku, kuwapatia vitambulisho na kuwaingiza kwenye kanzidata ili kupata takwimu za uhakika za maeneo wanayolima na kuiwezesha serikali kusimamia upatikanaji wa pembejeo kulingana na mahitaji yao.

Aidha, mipango mingine ni kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakati kwa kuweka utaratibu wa kumwezesha mkulima kujitegemea kwa pembejeo ili aache kuwa tegemezi wa mikopo ya mabenki yenye riba kubwa.

Pamoja na malengo hayo ya haraka, Wizara ya Kilimo inasimamia utekelezaji wa malengo ya muda mrefu yakiwemo Upatikanaji wa wanunuzi wapya wa tumbaku kwa sasa na kwa miaka ijayo kabla ya Juni, 2020, Kuongeza ubora wa zao la tumbaku kutoka asilimia 87 ya sasa hadi asilimia 92 ifikapo Juni 2022 na Kuongeza mbegu mpya na bora za tumbaku ili tuweze kupata masoko katika nchi nyingine kama vile China.

Alisema ili kufikia malengo hayo wadau wote wa tasnia ya tumbaku wanapaswa kushirikiana ili kufikia malengo hayo na wakulima kunufaika na jasho lao.

Tumbaku ni miongoni mwa mazao makuu ya kimkakati ya yaliyopewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mhe Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mazao mengine ni pamoja na Tumbaku,  Kahawa, Pamba, Korosho, Chai, michikichi na alizeti. 

Mhe Hasunga alisema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa malengo ya uzalishaji yanafikiwa kwa kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa pembejeo kwa wakati, kuboresha huduma za ugani na kutafuta masoko mapya ya tumbaku.

Waziri Hasunga amesema kuwa katika msimu wa kilimo 2019/2020 ambao masoko yake yataanza mwezi Mei 2020, kampuni za ununuzi zilizopo nchini ambazo ni Alliance One Tanzania, Premium Active Tanzania na Japan Tobacco International zimetoa mikataba ya kilo 42,225,985 na tayari wakulima wapatao 33,000 wameomba kusajiliwa na Bodi ya Tumbaku kutokana na uzalishaji huo. Uzalishaji huo ni mdogo na hivyo unaacha wakulima takribani 16,000 bila kulima tumbaku msimu huu.

Kutokana na hali hiyo, Wizara ya Kilimo kupitia Bodi ya Tumbaku ilianzisha jitihada za kutafuta masoko mengine ili kuziba pengo la kampuni ya Tanzania Leaf Tobacco – TLTC ambayo haijatoa makisio ya uzalishaji msimu huu.

Jihada hizo zimepelekea kupata kampuni nne (4) mpya ambazo zimeonesha nia ya kununua tumbaku ya Tanzania msimu ujao . Kampuni hizo Kampuni za Zambia kupitia kampuni ya kizawa ya MAGEFA GROWERS Ltd itanunua kilo 5,500,000, Kampuni ya TRANSAFRICQUE kupitia kampuni ya kizawa ya GRAND TOBACCO GROWERS Co. Ltd imeomba kununua kilo 9,000,000, Kampuni ya PETROBENA itanunua kilo 300,000, na Kampuni ya PACHTEC  Limited imeomba kununua kilo 500,000

Takwimu zinaonesha kwamba kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10 hadi kufikia mwaka 2016 tumbaku imekuwa na mchango mkubwa wa kuliingizia Taifa fedha za kigeni.  Kwa mfano katika mwaka 2017, tumbaku iliingiza fedha za kigeni kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 195.8 ikishika nafasi ya pili baada ya zao la korosho. Licha ya faida kwa taifa, pia, uzalishaji wa tumbaku unawanufaisha wakulima, wanunuzi, viwanda vya kusindika tumbaku, mabenki, wasambazaji wa pembejeo, Halmashauri za wilaya na wadau wengine katika mnyororo wa thamani.

MWISHO


from MPEKUZI

Comments