Taasisi Ya Saratani Ocean Road Yazidi Kuimarisha Huduma Zake Kwa Wananchi

Na Mwandishi Wetu, MAELEZO
SERIKALI kupitia Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) imenunua na kusimika mashine mbili za kisasa za huduma ya uchunguzi na tiba za kutibu saratani aina ya LINA na CT Simulator zenye thamani ya Tsh Bilioni 9.5/-  hatua inayolenga kupunguza muda wa kusubiri tiba mionzi kutoka wiki sita hadi kufikia wiki mbili.

Hayo yamebainishwa  leo Jumatatu (Desemba 2, 2019) Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dkt. Julius Mwaiselage  wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya ORCI katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano unaoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli.

Dkt. Mwaiselage alisema mashine hizo za kisasa zinazotumia teknolojia ya 3D zinapatikana katika hospitali yoyote kubwa ya saratani duniani kama India, Ulaya na Marekani, ambapo tangu mashine hizo zianze kutoa huduma za uchunguzi na tiba mwezi Septemba 2018 tayari wagonjwa 1,141 wamepatiwa matibabu.

‘’Kwa wagonjwa 1,141 waliotibiwa kwa kipindi hicho, takribani wagonjwa 208 wangepelekwa nje ya nchi kama  mashine hizi zisingekuwepo na hivyo Serikali imeweza kuokoa Tsh. Bilioni 10.4 ambazo zingetumika kutibu wagonjwa hao nje ya nchi ambapo mgonjwa mmoja hugharimu Tsh Milioni 50’’ alisema Dkt. Mwaiselage.

Dkt. Mwaiselage alisema mshine ya CT Simulator imesaidia kuanzisha huduma za kupima CT Scan katika taasisi hiyo ambapo hadi kufikia mwezi Septemba mwaka huu, jumla ya wagonjwa 1,430 walikuwa wamepata kipimo cha CT Scan, hivyo kupunguza usumbufu kwa wagonjwa ambao walitakiwa kwenda hospitali nyingine kupata huduma hiyo.

Kuhusu rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi, Dkt. Mwaiselage alisema katiks mwaka 2015, jumla wagonjwa 164 wa saratani walipatiwa rufaa kwenda nje ya nchi, lakini baada ya kuboresha huduma za saratani nchini, kuanzia  mwaka 2018 hadi 2019 ni wagonjwa 39 pekee waliosafirishwa nje ya nchi, ambapo wagonjwa hao wengi walikuwa wakienda nje kwa upasuaji na tiba mionzi ya kisasa.

Akibainisha mafanikio mengine, Dkt. Mwaiselage alisema ORCI pia imekarabati wodi mbili za kutolea tiba kemia ikiwemo kufungwa viyoyozi na kununua vitanda maalum vya kutolea tiba kemia hivyo kuongeza utoaji wa tiba kemia kutoka wagonjwa 40 kwa mara moja hadi wagonjwa 100 kwa mara moja, ambapo awali huduma hiyo ilikuwa inatolewa katika wodi 1 pekee.

‘’Kuongezeka kwa wodi na vitanda imesaidia kupunguza muda wa kuanza tiba kemia kutka siku 10 hadi tatu pekee, ikimaanisha mgonjwa anaweza kuanza tiba ndani ya siku tatu kama majibu ya vipimo vyake vyote vitakuwa sawa kupata tiba hiyo’’ alisema Mwaiselage.

Aidha Dkt. Mwaiselage anasema Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamiii, Jinsia na Wazee na Watoto imewezesha kuimarisha uhakika wa upatikanaji wa dawa kutoka asilimia 4 mwaka 2014/15 hadi kufikia  asilimia 95 mwaka 2018/19, na upatikanaji wa dawa upo kwa asilimia 100 kwa wagonjwa wenye saratani za mlango wa kizazi, matiti, Kaposi sarcoma, tezi dume, njia ya chakula, kooni, damu, matezi, ngozi na kibofu cha mkojo.

Akifafanua zaidi Dkt. Mwaiselage alisema asilimia 5 ya dawa  zinazopungua, hupatikana katika Duka la Dawa la Jamii la Taasisi ililolianzisha ili kuimarisha upatikanaji wa dawa za saratani na dawa zake hupatikana kwa bei nafuu sana ulikinganisha na maduka mengine ya binafsi.

Dkt. Mwaiselage alisema kuwa kutokana na kuimarika kwa huduma za saratani katika taasisi hiyo, wagonjwa kutoka nchi jirani za Kenya, Comoro, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na Burundi wameongezeka kuja kupata huduma za tiba saratani na hivyo kuongeza mapato ya Taasisi kwani wananchi wasio raia wanalipia huduma hizo.

MWISHO



from MPEKUZI

Comments