Serikali Yapinga Kuwafukuza Wakimbizi Wa Burundi

Na Abubakari Akida,MOHA
Serikali ya Tanzania imepinga tuhuma zinazoelekezwa kwake kwamba imekua ikiwafukuza wakimbizi kutoka nchini Burundi wanaoishi katika makazi na kambi mbalimbali katika mikoa ya Kigoma,Tabora na Katavi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Kangi Lugola katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam kikihusisha pande tatu;Serikali ya Tanzania,Serikali ya Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi(UNHCR),huku mkataba maalumu ukisainiwa na pande hizo tatu lengo ni kuwezesha urejeshwaji wa wakimbizi walioomba kurejea nchini kwao baada ya amani kurejea.

“Ni vyema tukaliweka hili wazi ili jumuiya za kimataifa na Mataifa mengine yajue kwamba tunaposema tunawarejesha wakimbizi wa Burundi sisi na Serikali ya Burundi tunachofanya ni kuhamasisha,kuhimiza wale ambao wako na hiari warudi Burundi,baada ya kugundua amani imerejea Burundi,sasa tunapofanya hivyo wenzetu wanatafasiri kwamba tunawafukuza wakimbizi,hiyo sio sahihi,serikali ya Tanzania na wananchi wake kwa ujumla wamekua wakipokea wakimbizi kutoka nchi mbalimbali na hatujaanza leo tumekua tukiwahifadhi na amani inaporejea wanaomba warejee katika nchi zao” alisema Lugola

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri wa Mambo ya Ndani kutoka nchini Burundi,Pascal Barandagiye amesemaBurundi sasa ina amani na wameona ipo haja ya raia wake warejee ili kuweza kuijenga nchi yao.

“Tunawahakikishia kwamba kama nchi tuna uwezo wa kupokea warundi 2000 kwa wiki na sisi tutahakikisha warundi wote wanarejea nyumbani,tutawafuata popote walipo,tunawahitaji warudi nyumbani ili tuje tujenge nchi yetu pamoja,” alisema Barandagiye

Kwa upande wa Kamishna Msaidizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi(UNHCR),George Okoth Obbo alisema wameshirikiana na nchi mbili za Tanzania na Burundi katika kuhakikisha yanakuwepo mazingira salama na yenye utu katika uendeshaji wa zoezi hilo huku akiwashukuru Watanzania kwa mwema wao wa kuendelea kuwapokea wakimbizi.

“Tanzania imekua nchi rafiki kwa wakimbizi,mawaziri wote wawili wamekubaliana suala la kurudi wa warundi nchini kwao,tuko hapa kuhakikisha zoezi hilo litaenda salama likizingatia ustawi wa pande zote tatu” alisema Okoth

Ni takribani mwezi mmoja umepita tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Magufuli kwenye ziara yake katika mkoa wa Katavi kuagiza pande zote zinazohusiana na masuala ya wakimbizi wakutane ili kuweza kujadili suala la warundi wanaojiandikisha kwa hiari kurudi nchini kwao,akiwaambia umefika wakati sasa wakurudi katika nchi zao kwenda kuzijenga   huku akiwaonya wakimbizi wanaoshiriki katika matukio ya uhalifu hapa nchini.


from MPEKUZI

Comments