Rais Magufuli Asimulia Alivyopewa SUMU Dodoma.....Ataja sababu ya kutowasifia sana wateule wake.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amesema kuwa hapendi kuwapongeza sana wateule wake, kwakuwa hatua hiyo ilimfanya achukiwe na viongozi wenzake alipokuwa Waziri wa Ujenzi baada ya yeye kupongezwa na Rais Mstaafu, Benjamini Mkapa alipofanya vizuri.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Novemba 12, 2019, wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa Kitabu cha Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, ambapo amesema anamshukuru kiongozi huyo kwa kuwa shujaa katika uongozi wake licha ya changamoto alizozipitia.

“Nakumbuka Mzee Mkapa pale tulipofanya kazi vizuri alifurahi na baadae akatamka mimi kuwa askari wake wa mwamvuli namba moja kwa kufanya kazi nzuri ya barabara, siwezi kusahahu suala hilo maishani mwangu kwasababu licha ya dhamira yake njema liliniletea mimi matatizo nilianza kuaona dalili za baadhi ya mawaziri tena wengine wa ngazi za juu kabisa kuanza kunichukia na baada ya hapo nikanyweshwa sumu Dodoma ambayo alimanusura iondoe uhai wangu lakini kwa neema za Mwenyezi Mungu nikakiepuka kifo.

“Baada ya tukio la kunusurika kifo nilimwendea Mzee Mkapa kumuelezea dhamira yangu ya kutaka kujiuzulu nakumbuka siku hiyo aliniangalia kwa jicho la baba na mwana akinihurumia na pia kunipa ujasiri na baada ya dakika chache aliniambia nanukuu “John kafanye kazi ukimtanguliza Mungu” na baada ya hapo nikapewa ulinzi nikaendelea kuchapa kazi,” amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli ameongeza kuwa, "Hilo suala lilinifunza sana hata mimi sasa hivi siwasifii sana wateule wangu, kwa sababu yasije yakawakuta yaliyotaka kunikuta mimi".


from MPEKUZI

Comments