Mabadiliko Sekta Ya Madini Yalilenga Kuweka Umiliki Kwa Watanzania-dkt. Kalemani

Asteria Muhozya na Tito Mselem, Dodoma
Imeelezwa kuwa Mabadiliko Makubwa yaliyofanywa na Serikali katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017, yalilenga kuhakikisha rasilimali madini inabaki mikononi mwa Watanzania  chini ya Usimamizi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani kwa niaba ya Waziri wa Madini ameieleza hayo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo katika Semina iliyolenga kuongeza uelewa  kwa Kamati hiyo kuhusu Kanuni mbalimbali zilizoundwa zinazohusu Sekta ya Madini na kuwasilishwa na Wataalam wa Sheria wa Wizara ya Madini wakiongozwa na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria , Edwin Igenge.
 
Kanuni zilizowasilishwa kwa kamati hiyo ni pamoja na Kanuni za Madini (Udhibiti wa Eneo la Mirerani),  Kanuni  zinazohusu  Biashara ya Almasi, Kanuni za Masoko ya Madini pamoja na  Marekebisho ya Sheria ya Madini.
 
" Mhe. Mwenyekiti kuna zaidi ya Kanuni 13 zilizoundwa amabazo zote zimelenga katika kurahisisha usimamizi wa Sekta ya Madini na kuwanufaisha Watanzania," amesema Dkt. Kalemani.
 
Aidha, ameongeza kuwa, masuala mengine ni pamoja na namna ambavyo watanzania wanashiriki katika umiliki wa asilimia 16  hadi 50  kwenye uwekezaji mkubwa katika sekta ya madini  na kueleza kuwa, awali suala hilo halikuwepo.
 
"Mhe. Mwenyekiti hii ndiyo sababu tuko hapa pamoja na Kamati yako ambayo inahusika moja kwa moja na masuala haya, ni masuala muhimu ambayo kamati yako inapaswa kuyajua," amesisitiza Dkt. Kalemani.
 
Ameongeza  suala ni usimamizi  wa sekta ya Madini kuwekwa chini ya Tume ya  Madini pamoja na  Serikali  kupitia Benki Kuu ya Tanzania kuwa  na akiba ya madini ya Dhahabu na kusema, "Mhe. Mwenyekiti suala hili lilikuwepo awali lakini sasa tumelirejesha tena''. 
 
Aidha, Waziri Kalemani amesema mabadiliko hayo yaliyofanywa katika sekta ya madini yamepelekea kupunguza nguvu ya wachimbaji wakubwa na kutoa nafasi kwa watanzania wengi kunufaika na rasilimali madini ikiwemo kuweka biashara ya madini wazi na uanzishwaji wa masoko ya madini ambayo yameleta manufaa kwa sekta.
 
katika hatua nyingine, Waziri Kalemani amesema kufuatia serikali kuweka mazingira mazuri  hususani kwa wachimbaji wadogo wa madini, serikali kupitia  Wizara ya Nishati imewezesha kufikisha nishati ya umeme kwenye migodi 32 ya wachimbaji wadogo wa madini suala ambalo linawawezesha kuchimba kwa faida na kuachana na matumizi ya mafuta. 
 
Naye, Makamu Mwenyekiti wa  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo William Ngeleja, akizungumza  katika semina hiyo ameipongeza Serikali hususan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa Maamuzi makubwa aliyoyafanya  katika Sekta ya Madini ambayo yalipelekea kufanyika kwa   Mabadiliko ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017 na kueleza kuwa, manufaa yake yanaonekana.
 
Pia, ameipongeza Serikali kwa uazishwaji wa Masoko ya Madini  pamoja na Ujenzi wa Ukuta unaozunguka Migodi ya Tanzanite Mirerani na kueleza kuwa, ukuta huo umeongeza tija kwa taifa kutokana na mapato yanayopatikana  baada ya udhibiti wa utoroshaji wa madini hayo  yanayopatikana Tanzania pekee ikiwemo usimamizi wa rasilimali hiyo.
 
" Mhe. Mwenyekiti kuna zaidi ya kanuni 13 zilizoundwa amabazo zote zimelenga ktika urahisisha usimamizi wa Sekta ya Madini na kuwanufaisha Watanzania, "
 
Vilevile, amesema semina hiyo imewaongezea weledi wajumbe wa kamati hiyo kuhusu mabadiliko ya  Sheria ya madini. Aidha, amempongeza Waziri Biteko kutokana na ushirikiano na usimamizi mzuri wa   rasilimali madini unaofanywa  na kusema  "Watendaji tembeeni vifua mbele mnaye kiongozi anayewawakilisha vizuri," amesema Ngeleja.
 
Pia, amechukua fursa hiyo kuipongeza Wizara ya Nishati  kwa usimamizi mzuri wa sekta ya Nishati na kusema kwamba,"Wewe Waziri Kalemani na mwenzio wa Madini mnamwakilisha vizuri Rais wetu sisi sote tunaona".
 
Aidha, kamati hiyo imeishauri Wizara  kuhusu masuala kadhaa yanayohusu sekta ya madini yakilenga katika kusimamia na kuboresha sekta  husika ili kuhakikisha kwamba rasilimali madini inawanufaisha  zaidi watanzania, ambapo Waziri Kalemani ameahidi kuufanyia kazi ushauri uliotolewa na kamat hiyo. Pia, kamati imeitaka wizara kuendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo  madini kuhusu masuala yanayohusu kodi pamoja na mambo mengine ya muhimu.
 
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula akijibu hoja zilizowasilishwa na Kamati hiyo, ameeleza kwamba, zipo tofauti  za kabla na baada ya kujengwa kwa Ukuta unaozunguka migodi ya Tanzanite Mirerani  na kueleza kwamba, mapato yameongezeka tofauti na ilivyokuwa awali. 
 
"Lakini Mhe. Mwenyekiti  sisi na wizara tunafanya kazi kama Timu, tunaendelea na  majukumu yetu ya usimamizi wa sekta ya madini lakini pia tayari serikali imetoa magari 36 , tumeongeza  watumishi  wapya 180  bado tunaendelea na kufanyia kazi lengo la kukusanya shilingi bilioni 470 kwa Mwaka wa Fedha 2019/20," amesema  Prof Kikula.
 
Kuhusu udanganyifu unaofanywa na baadhi ya vituo vya uchenjuaji dhahabu, amesema  Tume ya madini ilikwisha baini udanganyifu huo na suala hilo linadhibitiwa.
 
Wataalam wengine waliowasilisha Mada katika semina hiyo kutoka wizara ya madini ni pamoja na Maafisa Sheria Waandamizi Semeni Kakunda, Julieth Moshi pamoja na Afisa Sheria Godfrey Nyamsenda.
 
Wengine waliohudhuria semina hiyo ni  Wataalamu kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini.


from MPEKUZI

Comments