Zaidi ya watu Milioni 16 wajiandikisha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, 2019

Na. Angela Msimbira OR-TAMISEMI
 WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Selemani Jafo amesema hadi sasa uandikishaji wa orodha ya wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa umefikia watu milioni 16.9  kati ya malengo  yaliyowekwa ya watu milioni 22. 9 sawa na asilimia 74.

Mhe Jafo amesema hayo jana wakati wa kutoa tathimini ya uandikishaji wa Wapiga kura katika Orodha ya Daftari la wapiga kura katika kikao na waandishi wa habari kilichofanyika katika Ofisi za TAMISEMI Jijini Dodoma.

Mhe. Jafo amesema kumekuwa na hamasa kubwa kwenye uandikishaji baada ya viongozi mbalimbali hususani Wakuu wa Mikoa na wilaya kuingia mitaani kuhamasisha wananchi.

Mhe Jafo anafafanua kuwa Mkoa wa Dar es Salaam ukiongoza kwa kuandikisha wapigakura kwa asilimia 89. Wakati hali bado tete kwa Halmashauri ya Jiji la Arusha ambapo mpaka juzi  ikiwa ni siku ya kwanza tangu kuongezwa muda wa kuandikisha imeadikisha kwa asilimia 37 tu.

Amesema mpaka sasa wapiga kura 16,906,545  wameandikishwa ikiwa ni sawa na asilimia 74 huku Dar es Salaam iliyoandikisha kwa asilimia 89 ikiwa kinara ikifuatiwa na Pwani iliyoandikisha kwa asilimia 86, Tanga kwa asilimia 81, Mtwara kwa asilimia 80 na Lindi kwa asilimia 77.

Mhe. Jafo anaendelea kusema kuwa kwa upande wa Mikoa hakuna Mkoa ulioandikisha chini ya asilimia 50, hata hivyo Mkoa ulioandikisha chini zaidi ni Kigoma iliyoandikisha kwa asilimia 57, Kilimanjaro kwa asilimia 58, Arusha na Shinyanga kila mmoja ukiandikisha kwa asilimia 66.

Akifafanua kuhusu Halmashauri zilizofanya vibaya amesema hali ni mbaya kwa Halmashauri ya Jiji la Arusha ambayo imeanikisha kwa asilimia 37 na kufuatiwa na Halmashauri ya Moshi na Korogwe ambazo  kila mmoja imeandikisha kwa asilimia 51.

Awali akitoa tathimini ya uandikishaji wa siku saba za mwanzo zilizoishia Oktoba 14,  Mhe. Jafo amebainisha  wapigakura walioandikishwa walikuwa milioni 15.5 ambao ni sawa na asilimia 68 ya lengo la kuandikisha wapigakura milioni 22.9 huku Mkoa wa Pwani uliongoza kwa kuandikisha kwa wastani wa asilimia 80, ikifuatiwa na Dar es Salaam kwa asilimia 77, Tanga ikiandikisha kwa asilimi 76, Mtwara na Lindi kila mmoja kwa asilimia 75.

Pia Kilimanajro ilishika mkia kwa kuandikisha wastani wa asilimia 48, ikifuatiwa na Kigoma kwa asilimia 53 Arusha kwa asilimia 59.

Wakati huohuo Mhe. Jafo amesema anawashangaa  wanasiasa wanaobeza kuwa uchaguzi na uandikishaji wa mwaka huu ni wa kusuasua na kuwataka kuacha upotoshaji na kujikita kwenye takwimu za ukweli ambapo uandikishaji ulikuwa mkubwa ukilinganisha na uchaguzi wa mwaka 2014.

Amefafanua kuwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliopita, Watanzania zaidi ya milioni 11.49 (11,491,661) ikiwa ni asilimia 62 ya makadilio ya kuandikisha watu 18,587,742 walijiandikisha katika uchaguzi uliofanyika Desemba 14 mwaka 2014

Aidha, Mhe.Jafo amesisitiza kuwa watumishi wa umma hawalazimishwi kujiandikisha na kuwa hakuna hatua au adhabu yeyote  itakachochukuliwa kwa asiyejiandikisha na kuwa kinachofanyika ni kuhamasisha ili kuhakikisha demokrasia inachukua mkondo wake.

“ Kanuni za uchaguzi ziko wazi, hakuna mtu analazimishwa ila kinachotakiwa kufanyika ni watu kuhamasishwa. Tumeona sehemu zingine kuna maandamano ya pikipiki au magari ya kuhamasisha na hili jambo jema kwa nchi yetu, kujiandikisha kunampa fursa mtu ya kwenda kuchagua kiongozi, ukikosa fursa hiyo unaweza baadaye kulalamika umechangua kiongozi ambaye haleti maendeleo” Amesisitiza Mhe. Jafo

Akizungumzia kuhusu “clip za  video” zinazotembea kuwa asiojiandikisha atakosa fursa zingine za maendeleo,  amesisitiza kuwa kanuni  ziko wazi, suala la kujiandikisha na kupiga kura ni hiyari na  mambo haya siyo maelekezo ya Ofisi ya TAMISEMI, watu wanatakiwa kuambiwa faida za kujiandikisha na kupiga kura kwa mustakabali wa maendeleo  ya Taifa.

Hata hivyo, Mhe. Jafo amefafanua kuhusu taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii juu ya  watumishi wa Jiji la Dodoma kulazimishwa kujiandikisha  na kusema kuwa lengo lilikuwa ni kuwahamaisha watumishi kwasababu wao wanafanya kazi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa hivyo ni vyema wakawa mstari wa mbele kujiandikisha ili kuwahamasisha wengine kujiandikisha.




from MPEKUZI

Comments