Wadau Wa Uchaguzi Wakutana Jijini Dodoma Katika Maandalizi Ya Uboreshaji Daftari La Kudumu La Wapiga Kura.

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
TUME ya Taifa ya Uchaguzi na wadau mbalimbali wa Uchaguzi wamekutana jijini Dodoma kujadili juu ya uboreshaji wa Daftari lakudumu la wapiga kura ambapo imeeleza uboreshaji katika awamu hii utafanyika kwa kutumia teknolijia ya kieletroniki ya Biometriki (BVR) kama ilivyokuwa mwaka  2015..

Akiongea katika  mkutano huo wa wadau wa uchaguzi mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi,Jaji Semistocles Kaijage  amesema Teknolojia hiyo itachukua taarifa za mtu za kibaiolojia na kuzihifadhi katika kanzidata kwaajili ya utambuzi ,na ndio iliyotumika kuandikisha wapigakura mwaka 2015.

Pia amesema , uboreshaji wa safari hii hautohusisha wapiga kura wote waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga mwaka 2015 bali litahusisha wapiga  kura wapya ambao wametimiza umri wa miaka 18 na wale ambao watatimiza umri wa miaka 18 siku ya uchagauzi mkuu wa mwaka ujao 2020.

Kwa upande wake Mkurugenzi  wa uchaguzi Wilson Charles amesema kwa mujibu wa kifungu cha 10  cha sheria ya taifa ya uchaguzi sura  ya 343 na kifungu cha 15 cha sheria ya uchaguzi ya serikali za mitaa sura ya 292 inasema ili mtu aweze kuandikishwa kuwa mpiga kura anapaswa kuwa raia wa Tanzania.

Pia amebainisha ili mtu aweze kuandikishwa lazima awe na umri wa miaka 18 au zaidi au atatimiza umri wa miaka 18 kabla au ifikapo tarehe ya uchaguzi.

Hata hivyo amesema kuwa mtu anaweza kukosa sifa za kuandikishwa kama amethibitisha kuwa ana ugonjwa wa akili ,amehukumiwa adhabu ya kifo,anatumikia kifungo cha zaidi ya miezi sita ,amezuiliwa kujiandikisha kuwa mpiga kura na sheria za uchaguzi au sheria nyingine kwa makosa yanayohusiana na uchaguzi au hatakuwa ametimiza umri wa kupiga kura ifikapo siku ya uchaguzi.

Katika hatua nyingine amesema uzoefu inaonyesha kuwa katika chaguzi ndogo vyama vimekuwa havipeleki malalamiko yao kwenye kamati za maadili na badala yake vimekuwa vikipeleka malalamiko yao kupitia vyombo vya habari hali ambayo hupelekea malalamiko yao kutofanyiwa kazi na kamati za maadili.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma mara baada kukamilika kwa zoezi la kuapisha viongozi hao Kamishna wa Tume ya taifa ya uchaguzi Asina Omary amesema zoezi hilo ni la kisheria hivyo ni lazima taratibu zote za kisheria zifuatwe ili kulifanikisha   huku akizungumzia umuhimu wa uboreshaji wa Daftari hilo la wapiga kura.

Mkurugenzi wa idara ya usimamizi Tume ya taifa ya uchaguzi Anseem Mwampoma amewataka wananchi kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ili waweze kuchagua viongozi wanaowataka.

Ikumbukwe kuwa,Tume ya Taifa ya Uchaguzi imekamilisha uboreshaji wa Daftari awamu ya Kwanza katika mikoa ya Arusha,Kilimanjaro,Manyara,Simiyu,Mara,Mwanza,Geita,Shinyanga,Kagera  na Kigoma .

Hivyo kwa sasa zoezi hilo linaendelea katika mkoa ya Tabora,Katavi na Rukwa  na litaendelea mikoa mingine ikiwemo Dodoma.
Mwisho


from MPEKUZI

Comments