Mifuko ya Pamoja yamuenzi Mwl. Nyerere kwa kuchochea maendeleo

Na Mwandishi Wetu
OKTOBA 14, mwaka huu, Tanzania imeadhimisha miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa  Mwalimu Julius Nyerere.
 
Katika uhaki wake, Mwalimu Nyerere alikuwa na sifa ya utu, mpenda maendeleo, hakupenda kuona watu wakinyanyaswa, wakionewa au kupuuzwa kwa sababu za unyonge wao.
 
Mwalimu Nyerere alichukia rushwa, ufisadi, wizi na aina zote, kujenga misingi imara ya kulifanya Taifa lijitegemea, kutumi rasilimali zilizopo ili kujiletea maendeleo ya kweli.
 
Pia Mwalimu Nyerere alipenda kuona taasisi zilizoanzishwa na serikali zikiwakomboa Watanzania katika nyanja mbalimbali ili waweze kukuza mitaji, kipato chao na kulipa kodi stahiki.
 
Miongoni mwa taasisi iliyobeba maono ya Mwalimu Nyerere na kuyafanyia kazi kwa vitendo ni UTT AMIS.
 
Taasisi hiyo ipo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango iliyopewa dhamana ya usimamizi wa mali kupitia Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja. 
 
Utajiri siyo fedha ambazo mtu anakusanya bali ni fedha zinazowekwa na kufanya kazi. Tamaduni zetu zimeifanya jamii kubwa kuhifadhi fedha ndani katika vyungu, magodoro, vibubu.
 
Uwekaji akiba na uwekezaji ni dhana mbili tofauti. Uwekaji akiba ni mzuri lakini bila kuziwekeza ni bure. 
 
Ili uwe muwekaji akiba mzuri, unapaswa kuwa na nidhamu ya kujizoesha muda mrefu. 
 
Awali UTT AMIS ilipewa dhamana ya usimamizi wa mifuko mitano ambayo ni Mfuko wa Umoja, Wekeza Maisha, Watoto, Mfuko wa Kujikimu na Mfuko wa Ukwasi. Hivi sasa taasisi hiyo imeongeza mfuko mwingine wa Hati Fungani.
 
Nchini Tanzania unaweza kuwekeza fedha zako katika masoko ya fedha, mitaji. Hatua hiyo inahusisha akaunti za muda maalum na zisizo za muda maalum katika benki za biashara.
 
Pia hati fungani za Serikali za muda mfupi, mrefu, kampuni na hisa zilizoorodhosgwa katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) ambazo zina nafasi kubwa ya kurejesha gawio zuri. 
 
Uwekezaji unaofanywa na taasisi hiyo kupitia mifuko ambayo wanaisimamia ni fursa mbadala inayowezasha watu, vikundi, taasisi, kampuni kuwekeza pesa zao kwa Meneja wa UTT.
 
Meneja huzichukua fedha hizo, kuziwekeza kwenye masoko ya fedha, mitaji kulingana na waraka wa makubaliano.
 
Faida inayopatikana hugawanywa kwa wawekezaji kulingana na uwiano wa uwekezaji uliofanyika kwenye mfuko husika. 
 
Mfuko wa Umoja, ulioanzishwa Mei 16, 2005 ukilenga kutimiza mahitaji tofauti ya wawekezaji. Awali bei ya kipande ilikuwa sh. 70, kwa sasa sh. 590.2060.
 
Sifa zilizopo katika mfuko huo ni vipande kuuzwa kwa thamani halisi (hakuna gharama za kujiunga). kiwango cha chini cha kujiunga ni vipande 10 tu.
 
Malipo ya mauzo hutozwa asilimia moja ya thamani halisi, pia ni rahisi kujiunga, kutoka ambapo manunuzi na mauzo hufanyika kila siku ya kazi. 
 
Mfuko wa Watoto una lengo la kuwasaidia watoto katika maendeleo yao nchini. Awali bei ya kipande ilikuwa sh. 100, mfuko ulianzishwa Oktoba 1, 2008. 
 
Sifa za mfuko huo ni uwekezaji kwa ajili ya mtoto mwenye umri chini ya miaka 18. Kiwango cha chini cha uwekezaji sh. 10,000, unaruhusiwa kuwekeza kidogo kidogo kwa sh. 5,000.
Sifa nyingine ni vipande kuuzwa kwa thamani halisi (hakuna gharama za kujiunga), mfuko hutoa mipango ya aina mbili, kwanza malipo ya ada, pili mpango wa kukuza mtaji.
 
Malipo ya ada na mauzo ya vipande yanaruhusiwa pale mtoto anapofikisha miaka 12. Mfuko huo ni miongoni mwa mifuko  inayotatua changamoto za kielimu hasa katika ulipaji ada kwa wanafunzi, kutoa mtaji baada ya ukomo wa shule kufikia. 
 
Pia mfuko una mipango miwili mikubwa, mpango wa ada za shule na mtaji kwa mwanao. Ili mzazi aweze kuchangia kupitia mfuko huo, anapaswa kuweka sh. 10,000 kima cha chini na hakuna ukomo kwenye kiwango cha juu. 
 
Mfuko ulianzishwa mwaka 2008. Kiwango cha chini cha kipande kilianzia sh. 100, hivi sasa sh. 346.3151.
 
Mfuko wa Jikimu una lengo la kukidhi mahitaji ya wawekezaji wanaohitaji uhakika wa mapato ya mara kwa mara, ulianzishwa  Novemba 3, 2008 ukiwa na sifa za mipango ya uwekezaji, kiwango cha uwekezaji, mpango wa gawio robo mwaka.
 
Kiwango cha chini cha uwekezaji sh. milioni 2, mpango wa gawio wa mwaka (kiwango cha chini cha uwekezaji sh. milioni moja), tatu mpango wa mwaka wa kukua (sh. 5,000).Vipande vinauzwa kwa thamani halisi (hakuna gharama za kujiunga). 
 
Mfuko wa Ukwasi unaotoa nafasi ya uwekezaji mbadala kwa wawekezaji wakubwa au taasisi ambao wangependa kuwekeza fedha zao za ziada kwa kipindi kifupi ama cha kati huku wakikuza mtaji wao. 
 
Ulianzishwa Aprili 30, 2013, bei ya kipande ikiwa sh. 100.00, hivi sasa imepanda sh. 126.3239.
 
Sifa za mfuko huo ni rahisi mwekezaji kupata fedha zake za mauzo ya vipande ndani ya siku tatu za kazi baada ya maombi ya kuuza vipande kupokelewa Makao Makuu ya UTT AMIS.
 
Mfuko huo hauna ada ya kujitoa wala kujiunga, una unafuu wa gharama za uwekezaji, unafaa kwa wawekezaji mmoja mmoja au taasisi, kiwago cha chini cha kuwekeza sh. 5,000,000.00.
 
Kuongeza uwekezaji wako sh. 1,000,000.00, pia unaruhusu uhamishaji vipande kutoka kwa mwekezaji mmoja kwenda mwingine, kuruhuusu uhamishaji vipande kwenda kwenye mifuko mingine, kuviuza kwa thamani halisi.
 
Mfuko wa Wekeza Maisha unamwezesha mwekezaji kupata faida pacha (mapato mazuri pamoja na mafao ya bima). 
 
Mfuko huo ulianzishwa Mei 16,2007, wawekezaji kati ya miaka 18 na 55 ndio wanaoruhusiwa kujiunga. Unatoa mipango ya aina mbili, kuchangia uwekezaji awamu ya kwanza, mkupuo mmoja.
 
Vipande vinauzwa kwa thamani halisi, hakuna gharama za kujiunga. Kujiunga ni sh. 8,340.00 tu kwa mwezi. Bei ya kipande kwa sasa sh. 416.4499.
 
Mafao ya bima yanayopatikana ni bima ya maisha, ulemavu wa kudumu na bima ya ajali. 
 
Mfuko unamwezesha mwekezaji kuwekeza kwa mpangilio, kuchangia kwa mwezi, mara mbili kwa mwaka, mara moja kwa mwaka ambapo faida za uwekezaji katika Mifukoya Uwekezaji wa Pamoja ni kukuza mtaji kwa kutoa faida nzuri ukilinganisha na mifuko mingine kwenye masoko ya fedha.
 
Faida nyingine ni kutawanya hatari za uwekezaji, mwekezaji hupunguza athari za uwekezaji kwa kuwekeza katika uwekezaji auai, wawekezaji kufaidika na unafuu wa gharama za uwekezaji.
 
Pia wawekezaji wanaweza kufuatilia maendeleo ya masoko ya fedha kwa kufuatilia maendeleo ya mifuko.
 
Mfuko mpya Hati Fungani unaojulikana kama ‘Bond Fund’ ni kati ya mifuko ya uwekezaji wa pamoja inayoendeshwa na UTT AMIS ulioanzishwa kwa malengo maalum.
 
Kuanzishwa kwa Mfuko wa Hati Fungani kumetokana na mahitaji ya wawekezaji na uchambuzi wa bidhaa za kifedha zilizoko kwenye soko la mitaji kwa sasa. 
 
Mfuko utawawezesha wawekezaji wadogo na wa kati kuzifikia fursa za uwekezaji ambazo kwa hali ya kawaida ni wawekezaji wachache na wakubwa ndio wanaozifikia. 
 
Pia utawekeza kwenye hati fungani zilizoorodheshwa kwenye soko la hisa kwa asilimia 90 na asilimia 10 itakuwa kwenye uwekezaji wenye ukwasi mkubwa.
 
Lengo ni kuwawezesha wawekezaji wanaohitaji kuchukua fedha kutokana na uwekezaji wao katika mfuko wafanye hivyo. 
 
Mfuko umeundwa ili kumwezesha kila mwekezaji kuchagua kama anapenda kukuza mtaji au kupokea gawio kwa mwezi, kila miezi sita kutokana na mahitaji yake ya kifedha. 
 
Akiuzungumzia mfuko huo, Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa UTT AMIS, Daudi Mbaga, alisema umelenga  kuondoa changamoto ambazo wawekezaji wanakutana nazo.
 
Anasema soko la fedha lina bidhaa nyingi zilizobuniwa ili kukidhi mahitaji tofauti ya watumiaji. 
 
Baadhi ya bidhaa hizo zinaeleweka kirahisi hata namna ya kuzifikia na kuwekeza lakijni wakati mwingine hazitoi faida shindani kwa wawekezaji. 
 
Anasema baadhi ya wawekezaji hasa wadogo ni vigumu kuwekeza kwenye baadhi ya bidhaa katika soko la fedha. Mfuko wa Hati Fungani umeratibiwa ili kuondoa changamoto hizo. 
 
Mwekezaji anapata faida sawa na wawekezaji wakubwa, akihitaji fedha anauza baadhi ya umiliki wake kwenye mfuko kwa utaratibu rahisi bila kupoteza faida aliyoipata.
 
Pia mfuko huo unawafaa wawekezaji wakubwa kwa sababu ya faida shindani, gharama ndogo za kuwekeza, ukwasi wa kutosha, usalama wa mtaji, hatari ndogo za uwekezaji.
 
Mfuko unatoa fursa kwa wawekezaji kuwekeza, kushiriki katika masoko ya mitaji, kufaidika na uwekezaji huo. 
 
Kwa mantiki hiyo, mfuko umeandaliwa ili kutoa fursa kwa wawekezaji wa kipato cha chini, kati na kipato cha juu ambao ni watu binafsi, kampuni, taasisi na vikundi rasmi wanaweza kushiriki katika uwekezaji kwenye mfuko huo. 
 
Mbaga anasema, mfuko una mipango miwili ya uwekezaji ili kukidhi matakwa tofauti ya wawekezaji. 
 
Kuna mpango wa kukuza mtaji, gawio kila mwezi na gawio kila miezi sita, mpango wa kukuza mtaji.
 
Gawio la mara kwa mara halitatolewa kwa wawekezaji badala yake faida iliyopatikana itarudishwa kwenye uwekezaji wa awali kwa kununua vipande vitakavyonunuliwa kwa bei ya wakati huo. 
 
Mpango huo utawafaa wawekezaji wanaohitaji kuweka akiba kwa malengo maalum mfano kujenga nyumba au wafanyakazi wenye kipato kama wangependa kuwa na fedha ya akiba.
 
Wawekezaji katika mpango huo wanaweza kuuza kiasi chochote cha uwekezaji wakiwa wamekidhi vigezo vinavyohusu uuzwaji wa vipande.  
 
Wawekezaji wanaohitaji kuchukua faida kila mwezi kama  wastaafu wanaopata fedha zao za mkupuo, kuwekeza kwenye mfuko, wanashauriwa kuchagua kupokea gawio kila mwezi ili wapate kipato cha kuishi bila kupoteza fedha walizopata. 
 
Mbaga anasema wawekezaji wengine wanaopata fedha nyingi mara moja mfano wachimba madini, wanaweza kuchagua gawio kila mwezi ili wafanye shughuli zao bila kuathiri mtaji wao.
 
Pia wawekezaji watakaojiunga na mpango huo wanaweza kuuza vipande kidogo au vyote ili mradi wawe wamekidhi vigezo vya mfuko vinavyohusu uuzwaji vipande. 
 
Mpango wa gawio kila miezi sita, Mbaga alisema hutegemea na mahitaji ya fedha ya mwekezaji na anavyochagua kwenye fomu ya maombi ya kuwekeza kwenye mfuko. 
 
Kwa wawekezaji ambao wanahitaji kuchukua faida kila miezi sita mfano wafanyakazi wanaohitaji kuweka kiasi cha fedha ili faida inayopatikana itumike kulipa ada kusomesha watoto, wanaweza kuchagua kupokea gawio kila miezi sita. 
 
Pia kuna wawekezaji wanaopata fedha nyingi mara moja kama wakulima wa mazao mbalimbali ya msimu, wanaweza kuchagua kupata gawio kila miezi sita.
 
Wawekezaji watakaojiunga na mpango huo wanaweza kuuza vipande kidogo au vipande vyote ili mradi wawe wamekidhi vigezo vya mfuko.
MWISHO.


from MPEKUZI

Comments