Maombi ya Freeman Mbowe na Vigogo Wengine CHADEMA Yakataliwa

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetupilia mbali maombi ya upande wa utetezi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akiwemo mwenyekiti wake Freeman Mbowe juu ya kuanza kwa mashahidi wao kujitetea na badala yake wataanza kujitetea washtakiwa wenyewe.

Baada ya kutolewa uamuzi huo wakili wa utetezi, Peter Kibatala aliomba muda wa wiki tatu kwa ajili ya wateja wake kujiandaa kutoa utetezi huku akisema aliyekuwa tayari ni shahidi hivyo anaomba wateja wake wapewe muda wa kujiandaa.

Upande wa serikali ukiongozwa na Wakili Faraja Nchimbi umepinga muda huo ukisema hakuna sababu ya mahakama kuwapa muda huo hivyo hakimu kutokana na kuibuka kwa hoja hizo ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 21 mwaka huu atakapotoa uamuzi wa lini wataanza kujitetea.

Washtakiwa hao wanaanza kutoa utetezi wao baada ya mashahidi  nane wa upande wa mashtaka kutoa ushahidi wao na Mahakama kuwaona washtakiwa hao wana kesi ya kujibu wajitetee.

Wanaokabiliwa katika kesi hiyo,  mbali Mbowe ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar-Salum Mwalimu, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji.

Wengine ni wabunge; John Heche (Tarime Vijijini), Halima Mdee (Kawe), Ester Bulaya (Bunda Mjini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Esther Matiko (Tarime Mjini).

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendajia jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam


from MPEKUZI

Comments