Serikali Kuimarisha Mifumo Ya Ununuzi Wa Korosho.....Waziri Mkuu Asema Inalenga Kuvutia Wanunuzi Wa Ndani Na Nje Ya Nchi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema katika msimu wa ununuzi wa korosho wa mwaka huu ambao unatarajiwa kuanza hivi karibuni, Serikali imepanga kuimarisha mifumo ya ununuzi wa zao hilo ili kuvutia wanunuzi wengi zaidi kutoka ndani na nje ya nchi.

Pia, Waziri Mkuu amesema Serikaliitatoa nafasi ya kwanza ya ununuzi kwa wenye viwanda nchini, hivyo amewataka waandae mahitaji yao na kuyawasilisha kwenye mamlaka husika ili wawe na uhakika wa kupata malighafi ya kutosheleza mahitaji ya viwanda vyao.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Septemba 13, 2019) , wakati akiahirisha mkutano wa 16 wa Bunge la 11, Bungeni jijini Dodoma. Amesema wakulima wataarifiwa kuhusu utaratibu wa uuzaji wa zao hilo kwenye kikao cha wadau kitakachofanyika hivi karibuni.

Waziri Mkuu amesema Serikali imepanga kupanua soko la korosho kwa kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kutengeneza bidhaa nyingine zitokanazo na korosho zikiwemo siagi, maziwa, mvinyo na sharubati pamoja na kuendelea kujenga maghala ya mfano na yenye viwango kwa ajili ya kuhifadhia korosho katika maeneo ya kimkakati.

Ili kuhakikisha mpango huo unatekelezwa, Waziri Mkuu ameielekeza Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhakikisha zinasimamia upatikanaji wa masoko mapya ya mazao mbalimbali.

Amesema Wizara hizo, zinapaswa kuzingatia maelekezo mahsusi yaliyotolewa na Dkt. John Magufuli, alipokutana na Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi. Pia taasisi zinazohusika na utafutaji wa masoko ikiwemo Soko la Bidhaa (TMX), TanTrade na Bodi zote za Mazao zijielekeze katika kutafuta masoko ya mazao yanayozalishwa nchini.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa katika msimu wa 2018/2019 jumla ya tani 224,964 za korosho ghafi zenye thamani ya sh. bilioni 729.90 zilikusanywa. Kati yake tani 222,825 zilikusanywa na Serikali. “Korosho zilizolipwa ni tani 197,547 na Serikali inakamilisha malipo ya kiasi kilichobaki cha tani 25,278. Hivi sasa, korosho yote imenunuliwa na inasafirishwa. Aidha, baada ya zoezi hilo Bodi ya Mazao Mchanganyiko itarudi kulipa madeni yaliyobaki kwa wakulima na wenye maghala.”

Akizungumzia  ununuzi wa zao la pamba, Waziri Mkuu amesema mgogoro wa kibiashara kati ya mataifa makubwa umesababisha kuporomoka kwa bei ya pamba katika soko la dunia kinyume na matarajio kuwa bei ingeongezeka.

“Ili kukabiliana na hali hiyo, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kusimamia makubaliano kati ya Benki Kuu na Benki zilizotoa mikopo kwa makampuni yanayonunua pamba kulingana na mitaji yao ili  kununua pamba  yote  kwa wakati.”

Waziri Mkuu ametaja hatua nyingine kuwa ni pamoja na kuhamasisha kampuni hizo zipeleke fedha za malipo ya wakulima, kudhibiti udanganyifu kupitia mizani, kusimamia malipo ya wakulima na makato ya pembejeo katika maeneo yaliyobainika kutokea kwa vitendo hivyo.
 
Kuhusu zao la tumbaku, Waziri Mkuu amesema hadi kufikia tarehe 31 Agosti, 2019 mauzo ya tumbaku ya mkataba yalikuwa yamekamilika, huku jumla ya kilo milioni 60.59 zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 92.79 ilinunuliwa. Kiasi hicho, ni sawa na asilimia 105.7 ya lengo la kuzalisha kilo milioni 57.31 za tumbaku ya mkataba.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema tathmini ya masoko imeonesha uwepo wa tumbaku ya ziada kiasi cha kilo milioni 12.22 ambayo ilizalishwa nje ya mkataba katika maeneo mbalimbali. “Serikali inaendelea na majadiliano na makampuni ya ununuzi kwa lengo la kuhakikisha tumbaku yote inanunuliwa.”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Kilimo ihakikishe inawasimamia ipasavyo mawakala waliopewa jukumu la kusambaza pembejeo kwa wakulima ili ziwafikie wakulima kwa wakati na kwa bei inayohimilika na ubora unaohitajika.

Amesema katika kipindi cha kuanzia Septemba 2019 maeneo mengi nchini huanza kupata mvua za vuli ambazo ni ishara ya kuanza kwa msimu mpya wa kilimo, hivyo Serikali lazima ihakikishe wakulima wanapata pembejeo za kilimo ikiwemo mbegu bora, mbolea na viuatilifu kwa ajili ya msimu huu mpya wa kilimo.

Waziri Mkuu amesema hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula nchini imeendelea kuwa toshelevu. “Kwa mfano, katika msimu wa kilimo wa 2018/2019 uzalishaji ulifikia takriban tani milioni 16.41 ikilinganishwa na mahitaji ya tani milioni 13.84.”

Amesema hivi sasa wafanyabiashara wa mazao ya chakula wanaendelea kusafirisha na kuuza mazao hayo ndani na nje ya nchi. “Serikali inawahimiza wananchi wote wahifadhi chakula cha kutosha kwa ajili ya matumizi ya nyumbani hususan wakati huu tunapoingia kwenye msimu mpya wa kilimo kwa mwaka 2019/2020.”

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


from MPEKUZI

Comments