Mwanaharakati Cyprian Musiba Apewa ONYO Na Serikali....Akiendelea Atachukuliwa Hatua Kali

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Mhe.Kangi Lugola amemtahadharisha na Kumuonya Mwanaharakati huru  Cyprian  Musiba kuacha kuwaaminisha watanzania kuwa Serikali inamtumia.


Waziri Lugola amesema hayo leo Septemba 13,2019  jijini Dodoma Wakati akizungumza na Waandishi wa Habari ambapo amesema kuwa Mwanaharakati Cyprian Musiba anayemiliki pia gazeti la Tanzanite   serikali haimtumii na mambo yake hayabarikiwi na Serikali   bali ni matakwa yake binafsi.

“Kuna mwanaharakati huru Musiba anawadanganya watanzania kuwa serikali ina mtumia mpaka baadhi ya viongozi mbalimbali na Watanzania inafikia hatua ya kumwogopa,nataka kuwafahamisha watanzania serikali haimtumii endapo ataendelea kujigamba namna hiyo serikali itamchukulia hatua za kisheria”
Amesema Lugola.

Waziri Lugola amesema Musiba amekua akijaribu kuwaonesha na kuwaaminisha watanzania kwamba pengine Serikali imemtuma hivyo yeye kama Waziri mwenye dhamana ya mambo ya ndani ya Nchi anawahakikishia wananchi kwamba Serikali haiwatumi wanaharakati hao.

Amesema anafahamu kuwa wapo wanaharakati nchini wanaofanya harakati zao lakini amewaonya kuacha kufanya uwanaharakati unaopitiliza wa kuwaaminisha wananchi kuwa sisi viongozi tunabariki uwanaharakati wao.

" Nimuonye huyu Musiba kuacha kuhusisha harakati zake na Serikali au asiwaaminishe Watanzania kuwa Rais anamtuma, Serikali hatuwezi kufanya kazi kwa kuwatuma wanaharakati kutusemea.

" Kwa sababu imefikia hata wakati fulani viongozi wa Dini wanaandika waraka wakijaribu kumzungumzia huyu Musiba wanavyomuona na vitendo vyake kwamba wanadhani Serikali inabariki mambo yake. Niwahakikishie sisi hatujamtuma na tunamuonya mara moja kuacha harakati zake hizo," Amesema Waziri Lugola na kuongeza;

" Ninarudia akiendelea kujitanabaisha kwamba anatumwa na Serikali basi tutamchukulia hatua kali sana bila kuangaliana usoni wala kuoneana huruma"

Aidha,Waziri Lugola amewatahadharisha  baadhi ya watu ambao wamekuwa wakitumia majina ya viongozi na Mitandao kutapeli watu wengine ambapo amesema Serikali imejipanga kukabiliana na tatizo hilo.


from MPEKUZI

Comments