Erick Kabendera Asema Bado ni Mgonjwa, Mahakama Yatoa Maelekezo

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeamuru mwandishi wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera (39), ambaye hali yake ya kiafya bado ni tete, arudi mahakamani baada ya siku saba ili kupata taarifa ya matibabu.

Uamuzi huo ulitolewa leo saa tatu asubuhi wakati kesi hiyo ilipokuwa ikitajwa katika mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile.

Mahakama ilimpa nafasi Kabendera kuelezea maumivu anayosikia ambapo akijieleza alidai hali ya kushindwa kupumua usiku bado inaendelea na siku nane zilizopita alisikia maumivu makali mguu wa kulia, maumivu makali katika mfupa ndani ya paja hali inayomfanya akose usingizi.


Kabendera amesema  kuwa madaktari wa Gereza la Segerea walimpima damu na kumchoma Sindano tatu kutokana na tatizo la  kushindwa kupumua.
 
Amedai kuwa madaktari hao hawana vifaa vya kuwasaidia kugundua tatizo alilonalo hivyo, wamemshauri kufanya mazoezi.

Alidai mguu wa kulia na mfupa wa paja wa mguu huo una maumivu makali

Huku akionekana kuwa na maumivu makali, alidai alionana na daktari Alhamis iliyopita na juzi (jana) alimuona lakini hakumfanyia vipimo kwa sababu walikuwa na wageni hivyo, aliahidi kuonana naye leo.

“Nipo Segerea na kuna utaratibu wa madaktari kufanya matibabu kwa wagonjwa kila siku,” alidai.

Hatua ya Kabendera kueleza hayo ni baada ya Wakili wake, Jebra Kambole kudai kuwa hali ya mshitakiwa huyo inazidi kutetereka kwa sababu anashindwa kutembea vizuri na kushindwa kupumua.

Kambole amedai bado Kabendera hajafanyiwa matibabu vizuri kujua tatizo linalomsumbua na kuomba mahakama ielekeze magereza wampeleke hospitali yoyote ya Serikali ikiwamo Muhimbili ili wapate ripoti ya ugonjwa unaomsumbua.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai amewasiliana na Mkuu wa Gereza na kumueleza kuwa Kabendera anapatiwa matibabu na madaktari wamekuwa wakimuangalia mara kwa mara.

Amedai magereza wana utaratibu wao endapo wataona ugonjwa unaomsumbua unahitaji rufaa, watampeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Rwizile ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 18, mwaka huu 2019 na kumuelekeza Kabendera kuonana na daktari kisha itakapotajwa tarehe nyingine ataieleza mahakama kama amepata matibabu au la ili mahakama itoe maelekezo.


from MPEKUZI

Comments