Bunge Lapitisha Sheria Kuwabana Wanaotuma au kusambaza picha za maiti au waathirika wa ajali.

Bunge limepitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 6 wa Mwaka 2019, ambao pamoja na mambo mengine, upendekeza kuifuta Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA).

Muswada huo pia unapendekeza kuweka adhabu kali dhidi ya watu wanaotumia au kusambaza picha za maiti au waathirika wa ajali.

Akiwasilisha muswada huo unaopendekeza marekebisho katika sheria tisa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Prof. Adelardus Kilangi, alisema mabadiliko hayo yanahusisha Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16 iliyotungwa mwaka 1930 kwa lengo la  kuainisha adhabu kwa makosa mbalimbali.

Alisema tangu kutungwa kwa sheria hiyo, imerekebishwa mara 67 kupitia sheria mbalimbali na marekebisho ya sasa yanalenga kuongeza adhabu ya faini kwa makosa chini ya kifungu cha 29 ili kuondoa adhabu zilizopitwa na wakati kutokana na hali ilivyo sasa.

"Kifungu kipya cha 162 kinapendekezwa kuongezwa ili kutoa adhabu kwa watu wanaotumia na kusambaza picha au video za maiti, waathirika wa majanga na matukio ya kutisha yanayohatarisha amani au kuingilia utu wa mtu," alisema.

Alisema katika muswada aliouwasilisha jana, marekebisho yanalenga kuifuta SSRA na kuhamisha jukumu la usimamizi wa sekta ya hifadhi ya jamii kwenda kwenye divisheni inayowajibika kwa masuala ya hifadhi ya jamii.

"Muundo wa kitaasisi uliopo sasa kwenye Sheria ya SSRA, Sura ya 135 unapendekezwa kufutwa na badala yake majukumu ya usimamizi wa sekta ya hifadhi ya jamii kuhamishiwa kwenye divisheni hiyo," alisema.

Prof. Kilangi alisema eneo la usimamizi wa masuala ya fedha na uwekezaji wa mifuko litaendelea chini ya uangalizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kama ilivyo sasa.


from MPEKUZI

Comments