Yaliyojiri wakati Rais Magufuli na Rais Ramaphosa walipozungumza na wananchi wa Tanzania na Afrika Kusini kupitia vyombo vya habari

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amemuomba Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Matamela Cyril Ramaphosa kuwahamasisha zaidi wafanyabiashara wa Afrika Kusini kuja kuwekeza hapa nchini kwa kuwa Tanzania inayo dhamira ya dhati ya kuongeza ushirikiano wake na nchi hiyo katika nyanja mbalimbali za kiuchumi.

Rais Magufuli amesema katika kutekeleza mipango yake ya maendeleo na dira ya kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 Tanzania inawakaribisha wawekezaji mbalimbali, kwa kuwa Afrika Kusini imepiga hatua kubwa katika viwanda amewaalika wafanyabiashara wa nchi hiyo kuja kujenga viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo dawa na vifaa tiba, kuchakata madini na kwamba Serikali itatoa ushirikiano wowote utakaohitajika.

Rais Magufuli pia amemuomba Rais Ramaphosa kuongeza ushirikiano na Tanzania katika utalii, hasa ikizingatiwa nchi hiyo inapokea watalii zaidi ya Milioni 10 kwa mwaka ikilinganishwa na Watalii Milioni 1.5 wanaoingia hapa nchini, na katika hilo ametoa wito kwa Afrika Kusini kuongeza safari za treni ya watalii na kwa wawekezaji wake kuja kuwekeza katika hoteli na fukwe za Tanzania.

Amempongeza Rais Ramaphosa kwa kuja na wafanyabiashara ambao wanajadiliana na wafanyabiashara wa Tanzania juu ya kushirikiana kibiashara, na amemhakikishia kuwa Tanzania itakuwa tayari kuhakikisha ushirikiano huo unafanikiwa.

“Sisi Tanzania tumeamua kuwa tunanunua bidhaa zetu Afrika Kusini badala ya kununua bidhaa hizo huko mbali, na kwa kuanzia pikipiki za kuongozea misafara ya viongozi tutakazotumia wakati huu wa Mkutano wa 39 wa SADC tumenunua Afrika Kusini” Rais Magufuli.

Kwa upande wake Rais Ramaphosa amemshukuru Rais Magufuli kwa kumwalika kufanya ziara ya Kitaifa hapa nchini na amemhakikishia kuwa wananchi Afrika Kusini wanaiona Tanzania ni nyumbani kwao na hivyo Serikali yake ipo tayari kuuendeleza na kuukuza uhusiano mzuri kati yake na Tanzania.

Rais Ramaphosa ameelezea kufurahishwa kwake na kuwepo kwa kampuni 228 za Afrika Kusini zilizowekeza nchini Tanzania na kuajiri wa zaidi ya watu 21,000 na ameahidi kwenda kuwahimiza zaidi wafanyabiashara na wawekezaji wa Afrika Kusini kuja kuwekeza nchini Tanzania huku akiwakaribisha wawekezaji wa Tanzania kwenda kuwekeza Afrika Kusini.

Aidha, Rais Ramaphosa amesema Afrika Kusini ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika nyanja nyingine mbalimbali zikiwemo afya, ulinzi na usalama, utalii na amekubaliana na mapendekezo ya Tanzania juu ya mpango wa kufundisha lugha ya Kiswahili nchini Afrika Kusini hasa wakati huu ambapo SADC inatarajia kuifanya kuwa lugha rasmi ya 4.

==Taarifa ya Ikulu


from MPEKUZI

Comments