Waziri Mkuu Azindua Mwongozo Wa Uwekezaji Kagera ....Azitaka Halmashauri Nchini Kuondoa Urasimu, Vikwazo Kwa Wawekezaji

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amezindua Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa wa Kagera wenye lengo la kutangaza fursa za Uwekezaji na hivyo, kukuza maendeleo ya mkoa huona ameziagiza halmashashauri zote za wilaya nchini ziondoe urasimu na kupunguza vikwazo kwa wawekezaji.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Agosti 14, 2019) wakati akizindua Kongamano la Wiki ya Kagera na Mwongozo wa Uwekezaji mkoani Kagera, lilifanyika Bukoba mjini.Amewataka Watanzania wahakikishe wanachangamkia fursa za biashara zilizopo.

Amesema Watanzania wanao uwezo wa kutumia fursa za uwekezaji na biashara zilizopo nchini kwa kushirikiana na taasisi za kifedha na kuwekeza katika miradi mbalimbali nchini, badala ya kuachia fursa hizo kuchukuliwa na wageni.

Amesema azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ya kukuza uchumi kupitia sekta ya na kufikia wa kati ifikapo mwaka 2025 itaendelea kutekelezwa, hivyo, ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wa nje nao waje kuwekeza.

“Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda Awamu ya Tatu (2010/2020) na Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2015/2016 2020/2021) ambao lengo lake ni kuendeleza uchumi wa viwanda”.

Akizungumzia kuhusu maadhimisho ya Wiki ya Uwekezaji Kagera, Waziri Mkuu amesema yamelenga kuwakutanisha wadau wa uwekezaji, ambao ni pamoja na Wafanyabiashara kutoka ndani ya mkoa na nchi jirani zinazozunguka Mkoa wa Kagera.

“Ni ukweli usiofichika kwamba tunahitaji wawekezaji watakaosaidia uchumi wa mkoa huu kukua kwa kasi kupitia fursa zilizopo kwenye nyanja za kilimo, mifugo, uvuvi, viwanda, maliasili na utalii”.

Waziri Mkuu amesema ukuaji mzuri wa uchumi wa mkoa utakuwa na manufaa katika kuongezeka kwa pato la mwananchi wa Kagera, pato la mkoa na hata pato la Taifa nalo litakuwa kwa kasi ndani ya kipindi cha muda mfupi.

Amesema mkoa wa Kagera ndiyo unaoongoza kwa uzalishaji wa kahawa nchini, ambapo zaidi ya nusu ya kahawa yote huzalishwa katika mkoa huo. Wastani wa uzalishaji wa kahawa kwa mwaka ni kati ya tani 50,000 hadi tani 65,000 kutegemea na hali ya hewa ya mwaka husika.

Hivyo, mkoa huo una fursa kubwa ya uwekezaji kwenye viwanda vya kukoboa na kusindika kahawa.Pia mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa michache Tanzania yenye fursa nyingi za uwekezaji ambazo kwa namna moja au nyingine hazipatikani katika mikoa mingine ya nchini. Miongoni mwa fursa hizo ni pamoja na soko kwani unapakana nan chi nne za Afrika Mashariki.

“Kagera imepakana na Uganda, Rwanda, Burundi na Kenya. Kupakana na nchi hizo zenye idadi kubwa ya watu katika ukanda huu wanaokadiriwa kufikia takriban milioni 190 ambapo kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2018 ni fursa ya uwepo wa soko kubwa la bidhaa zinazozalishwa au zinazoweza kuzalishwa katika mkoa wa Kagera”.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuboresha miundombinu mbalimbali ya usafiri ukiwemo wa anga na wa barabara ili kurahisisha usafiri kutoka Bukoba makao makuu ya mkoa wa Kagera kufika katika nchi hizo.

“Kwa mfano, umbali kutoka Bukoba hadi Kampala ni km. 340, Bujumbura km. 550 na Kigali km. 490. Kadhalika, itakuwa ni rahisi kufikia masoko ya nchi za Sudan Kusini pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo (DRC)”.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti alisema dhamira ya kuandaliwa kwa wiki ya uwekezaji mkoani Kagera ina lengo la kuhakikisha kwamba mkoa huo unafanya vizuri katika sekta ya uwezekezaji na biashara, hivyo kuchangia katika ukuaji wa pato la Taifa.
 
Alisema mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa 10 ambayo inamchango mdogo katika pato la Taifa, hivyo wanataka watoke kwenye kuchangia asilimia 3.9 hadi wafikie asilimia 10.

Kwa upande wao, viongozi mbalimbali wakiwemo Magavana kutoka na wafanyabiashara kutoka nchi za Rwanda na Burundi waliahidi kutumia fursa zilizopo nchini, pamoja na kuwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania kwenda kuwekeza katika nchi zao.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,        
JUMATANO, AGOSTI 14, 2019.


from MPEKUZI

Comments