Waziri Jafo Aingilia Kati sakata la watumishi wa Hospitali kulipishwa mashine ya Ultrasound iliyoibiwa

Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jafo ameingilia kata sakata la watumishi wa Hospitali ya Mji wa Bariadi  na kuamruru wasichangishwe fedha kufidia mashine ya Ultrasound iliyoibwa hospitalini hapo.

Jafo ametoa kauli hiyo jana Alhamisi Agosti 15, kauli ambayo inamuunga mkono Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini ya kutaka watumishi hao wasilipishwe fedha kama walioamriwa na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga  Jumatano Agosti 14.

Pamoja na mambo mengine, Jafo amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka kuunda tume ya uchunguzi ili kuwabaini waliohusika na wizi wa mashine hiyo.

“Kulikuwa na maelekezo kuwa wale watumishi 137 walipie ile mashine kwa kukatwa kwenye mshahara yao, nielekeze kwamba watumishi wetu hawa wanafanya kazi katika mazingira magumu sana, na tukumbuke hata tulipopata janga pale Morogoro watumishi wetu wa idara ya afya muda mwingi ndiyo walikuwa kimbilio kuwasaidia wananchi.

“Kitendo kama hiki ni kuwakatisha tamaa na kuwaweka katika ya sintofahamu lakini kumbe inawezekana kuna watu walihusika. Lengo hapa ni kuwatafuta waliohusika, wabainishwe ni kina nani wachukuliwe hatua lakini pia wahakikishe mashine hii inarudi.

“Kwa hiyo nitoe maelekezo kuwa watumishi hawa wasichangishwe fedha ya aina yoyote kwa sababu siyo jukumu lao, ni jukumu la ulinzi kwa hiyo Mkuu wa Mkoa namuelekeza kwanza aunde tume ya uchunguzi kuwabaini wahusika na watumishi hao waachwe wafanye kazi kwa sababu tunawategemea sana haipaswi kuwabebesha mzigo usiowahusu,” amesema Jafo.

Mashine hiyo inadaiwa kuibiwa pamoja na kifaa chake cha kudurufu picha (printer) ambapo ilikua maalumu kwa matumizi ya wodi mpya ya akina Mama wajawazito na iliibiwa ikiwa katika wodi hiyo.


from MPEKUZI

Comments