RAS Simiyu Asitisha Uamuzi Wa Dc Kuwataka Watumishi Kuchangia Fedha Za Kununua Mashine Ya Ultrasound Iliyoibiwa Bariadi

Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Uongozi wa Mkoa wa Simiyu kupitia kwa Katibu Tawala wa Mkoa, Bw. Jumanne Sagini umesitisha uamuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga, uliotolewa jana Agosti 14, 2019 ambapo watumishi wote 137 wa Hospitali ya Mji wa Bariadi walitakiwa kukatwa mishahara yao kwa ajili ya kuchangia fedha ya kununua mashine ya ULTRASOUND, iliyoibiwa katika wodi ya wazazi hospitalini hapo  badala yake ameagiza vyombo vya dola vifanye uchunguzi kubaini aliyeiba mashine hiyo na hatua stahiki zichukuliwe.

Sagini ameyasema hayo leo Agosti 15, 2019 wakati akizungumza na watumishi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bariadi katika Ukumbi wa Hospitali hiyo Mjini Bariadi.

Amesema uongozi wa Mkoa umetafakari na kuona kuwa si watumishi wote wa hospitali hiyo wamehusika katika upotevu wa mashine hiyo kwa kuwa wanafanya kazi katika idara tofauti na baadhi yao siku ya tukio hawakuwepo, hivyo ni vema vyombo vya dola vikafanya uchunguzi kubaini waliohusika.

" Uongozi wa Mkoa tunarekebisha baadhi ya hatua zilichukuliwa na Mhe. DC jana, hili jambo haliwezi kuwa la watumishi wote 137, kama Serikali tunavyo vyombo vya dola ambavyo kuna watu wanalipwa mishahara kwa kazi hizo za kiuchunguzi, tunataka kifaa hicho kirejeshwe, vyombo hivi vifanye uchunguzi, vichukue hatua kwa watakaobainika ikiwemo kupelekwa mahakamani" amesema.

Katika hatua nyingine Sagini amewataka watumishi wa Hospitali ya Mji wa Bariadi kuimarisha mfumo wa makabidhiano ya kazi na vifaa vya kazi ili kuwepo na taarifa sahihi za wagonjwa na vifaa tiba kama utaratibu unavyotaka.

Kwa upande wao watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi wamewashukuru viongozi wa Mkoa wa Simiyu  kwa kusitisha uamuzi wa awali ambao ungewaathiri kiuchumi na kupunguza ari ya kufanya kazi hususani wale ambao hawajahusika na upotevu wa mashine hiyo.

" Tunamshukuru sana kiongozi wetu kwa msamaha aliotutolea  kwa sababu tangu jana tumelala kwa presha baada ya kuambiwa kuwa kila mtu alip, mimi uwezo wangu mdogo na mshahara wangu ni mdogo nilikuwa sioni pesa ya kulipa hicho kifaa;namshukuru Mungu kwa uamuzi wa viongozi wa mkoa yaani naongea kwa uchungu mpaka nasikia kulia kwa furaha niliyonayo" amesema Frola Katoyo Mtumishi katika idara ya dawa.

"Nimepokea vizuri uamuzi uliofanywa na viongozi wetu wa mkoa kwa sababu maanuzi yaliyotolewa jana kiuhalisia si kila mtumishi alipaswa kuhusishwa kwenye hili, maana wengine walikuwa likizo, wengine hawakuwepo kazini, hivyo ni sahihi kabisa kuviachia vyombo vya dola; nina uhakikia kuanzia leo watu watafanya kazi maana jana utendaji kazi ulipungua baada ya kupata tu taarifa kuwa wanapaswa kuchangia" alisema Simon Chisomeko Afisa Afya.

Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Mkoa wa Simiyu, Bi. Catherine Nyingi amesema Chama hicho kinaushukuru uongozi wa mkoa kwa kutambua sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma na wameiomba Serikali iendelee kuwa macho katika kusimamia sheria, kanuni na taratibu.

Mashine ya kupima magonjwa ya ndani ya mwili wa Binadamu (ULTRASOUND MACHINE) iliripotiwa kuibiwa katika Wodi ya wazazi katika Hospitali ya Mji wa Bariadi  Agosti 05, 2019 na jana Agosti 14, 2019 Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga akaagiza watumishi wote 137 wa Hospitali hiyo wakatwe fedha kwenye mishahara yao ili mashine hiyo iliyoibiwa  inunuliwe.


from MPEKUZI

Comments