Rais wa DRC Felix Tshisekedi Aiomba Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) Isaidie Kulidhibiti Kundi la MTN Na Ugonjwa wa Ebola

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) zimeombwa kuchukua jitihada kukabiliana na matishio ya ugaidi na ugonjwa wa Ebola.

Maombi hayo yaliwasilishwa na rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wakati wa mkutano wa 39 wa jumuiya hiyo unaoendelea nchini.

Rais Tshisekedi alisema nchi yake bado imeendelea kukabiliwa na matishio ya usalama hasa katika eneo la Mashariki kutokana na kuwapo kwa kikundi cha MTN ambacho kinatumia mfumo wa kushambulia kwa mtindo wa ugaidi.

“Ndiyo maana nilitengeneza mkakati wa kuimarisha mamlaka ya serikali ili kuzuia kundi hili kuendelea na tumeweka mfumo wa mapatano kwa makundi yote ili kusaidia kurejesha amani.

“Mtusaidie tuwe na mshikamano ili kupitia kwenu tutoke na tamko litakalosaidia kuimarisha kundi la Monusco (Majeshi ya walinda Amani ya Umoja wa Mataifa) ili liweze kukabiliana na makundi hasimu,” alisema Rais Tshisekedi.

Pia aliziomba nchi wanachama kuunda kundi la kikanda litakalosaidia kutokomeza vikundi vya kigaidi ambavyo vimekuwa tishio kwa baadhi ya nchi.

Kuhusu ugonjwa wa Ebola alisema wanashirikiana na Shirika la Afya duniani  (WHO) na tayari wamechukua hatua mbalimbali kuudhibiti na kutaka nchi wanachama kuendelea kuwasaidia kuudhibiti.

Pia alizihimiza nchi wanachama kuendeleza ujenzi wa mabwawa ya kuzalisha umeme ili kuwa na nishati ya kutosheleza mahitaji ya Sadc.

“Katika suala la kilimo nchi zetu zina fursa nyingi sana na sisi tuko tayari kwa ajili ya utekelezaji wa mikakati mbalimbali, naamini mkutano huu wa marais na viongozi wa serikali utafikia uamuzi thabiti wa kuhakikisha kunakuwa na mazingira wezeshi ya kuimarisha viwanda ili kuwa na maendeleo jumuishi,” alisema.


from MPEKUZI

Comments