Msemaji Mkuu wa Serikali: Nchi 16 Zimethibitisha Kushiriki Mkutano Mkuu Sadc Tanzania 2019

Na. Mwandishi Wetu-MAELEZO
Nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) zimethibitisha kushiri Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hiyo utakaofanyika  Jijini Dar es Salaam, Tanzania  Agost 17 na 18 mwaka huu.

Akizungumza katika Kipindi cha 360 cha Clouds Tv, Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt.Hassan Abbasi alisema maandalizi yamekalika na sasa Tanzania iko tayari kwa ugeni huo.

Dkt. Abbasi alisema kuwa mkutano huo ulitanguliwa na matukio mbalimbali ikiwemo Maonesho ya Wiki ya Viwanda kutoka nchi wanachama wa SADC, Vikao vya Maafisa Waandamizi kutoka SADC, Vikao vya Mawaziri kutoka SADC na Mikutano mbalimbali ya sekta za SADC, ambapo maeneo haya yote Tanzania inachukua uenyekiti wa Nchi Wanachama.

“ Katika mikutano yote iliyotangulia karibu nafasi zote za SADC kuanzia zile za kusimamia kamati, kusimamia mabaraza mbalimbali, Tanzania imechukua hatamu, kwani kuna sekta nyingi sasa zimeshachukua uenyekiti, Juzi Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania  alichukua kiti hicho cha  kwenye kamati ya wanachama wa SADC, vilevile Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania naye alichukua nafasi hiyo kwenye Kamati ya Mawasiliano SADC”, Dkt. Hassan Abbasi.

Dkt.Abbasi alisema kuwa kuelekea kwenye tukio lenyewe ambalo ni Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Wafalme kutoka Serikali 16 za nchi wanachama, zimethibitisha kushiriki mkutano huo na kuwa viongozi wao wataanza kufika nchini kuanzia tarehe 15 na kuendelea.

Aidha Dkt.Abbasi alisema kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa Kitovu cha Amani kwa nchi za kusini mwa Afrika, kwa hiyo viongozi wengi wa nchi hizo watakuja Tanzania kama wanarudi nyumbani, ambako ni kituo cha ukombozi wa nchi zao, na kufanya mkutano ambapo Agost 17 na 18 Wakuu wa  Nchi Wanachama watasaini mikataba mbalimbali na kuhitimisha ajenda zao.

Aliongeza kuwa kabla ya kufika mkutano wa wakuu wa nchi kuna matukio mengine kama vile Mabalozi na wawakilishi wa Tanzania kutoka nchi mbalimbali kuwasili nchini; ikiwa ni lengo la kushiriki Mkutano Mkuu ambapo pia wamepata wasaa wa kufanya ziara katika miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ya Awamu  ya Tano.

“Kabla ya kufika Mkutano Mkuu, kuna matukio mbalimbali ambayo pia ni makubwa na ni muhimu sana kwa nchi yetu, leo tunatukio kubwa la Mabalozi 42 wa Tanzania kutoka nchi mbalimbali duniani wanatembelea mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere Hydro Power Project( JK HPP) na kesho watatembelea mradi wa Ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR) na hawa wote wako nchini kwa ajili ya kushiriki Mkutano Mkuu wa SADC”, Alisisitiza  Dkt.Abbasi.

Dkt.Abbasi alisema kuwa Mabalozi hao wamekwenda kuona kwa mfano, ni nini serikali yao inatekeleza ili wakirudi katika maeneo yao ya kazi wapate kuyatangaza waliyoyaona na kuweza kuleta wawekezaji watakao kuja kuwekeza nchini na kuleta mapato kwa taifa.

Pia, Dkt. Abbasi alisema kuwa leo Tanzania itampokea  Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ambaye atawasili nchini kwa ziara ya siku mbili kabla ya Kusiriki Mkutano Mkuu, na ziara yake itajikita zaidi katika kutembelea eneo la wapigania uhuru Mazimbu, Mkoani Morogoro, ili kujenga kumbukizi ya Udungu kati ya Tanzania na Afrika Kusini.


from MPEKUZI

Comments