Katibu Mkuu CCM Dk. Bashiru Ally Awajulia Hali majeruhi waliopata ajali ya moto wa lori la mafuta Morogoro

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amesema ni vyema Serikali ikaona umuhimu wa kutenganisha barabara za kupita magari ya mizigo na ya kawaida ili kuepusha hatari kwa wananchi.

Dk. Bashiru aliyasema hayo jana wakati alipotembelea majeruhi waliopata ajali ya moto wa lori la mafuta lililoanguka mkoani Morogoro.

Mbali kutembelea majeruhi waliolazwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, pia alitembelea chumba cha kuhifadhia maiti, kuomba dua makaburini na eneo la Itigi-Msamvu ambako lori hilo lilipinduka kabla wananchi hawajalivamia kuiba mafuta na baadaye moto kulipuka.

Alisema kutenganishwa huko kutasaidia magari makubwa kutopita maeneo ya makazi ya watu na hata kukitokea majanga kama ya moto, wananchi hawataweza kupata madhara.

Hata hivyo, aliishauri Serikali kuweka utaratibu wa kutoa elimu ya majanga ya moto ili wananchi waweze kuwa na uelewa mara zote na kuweza kukaa mbali na matukio ya moto ikiwemo yanapoanguka magari ya mafuta.
Katibu Mkuu wa CCM Dk. Bashiru Ally (katikati) na Katibu wa CCM mkoa wa Morogoro Ndg. Shaka Hamdu Shaka (wa kwanza kushoto) wakiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro leo Agosti 14, 2019 ambapo wamewajulia hali majeruhi wa ajali ya moto waliolazwa katika hospitali hiyo


from MPEKUZI

Comments