Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC) Chatakiwa Kuwajengea Uwezo Maafisa Mipango

Na Peter Haule, WFM, Dar es Salaam
Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC) kimetakiwa kutoa mafunzo ya takwimu rasmi za Serikali kwa maafisa mipango nchini ili kuwajengea uwezo wa kufuatilia na kufanya tathimini ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka Mitano katika maeneo yao ya kazi.

Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam na  Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, alipofanya ziara katika Chuo hicho ikiwa ni sehemu ya kufuatilia utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19  katika Chuo hicho.

Alisema kuwa mafunzo ya takwimu rasmi za Serikali yanatakiwa kutolewa kwa Maafisa Mipango  kuanzia ngazi ya Serikali Kuu hadi Serikali za Mitaa ili kuwezesha kufanya tathimini ya mipango ya maendeleo na kuweka mikakati yenye tija kwa taifa hususani kwa wananchi wa hali ya chini katika kukuza kiwango chao cha maendeleo katika nyanja ya uchumi, kijamii na masuala ya sayansi na teknolojia.

“Wizara ya Fedha na Mipango inayonafasi kubwa ya kuhakikisha Chuo hiki kinajiimarisha katika Sekta ya miundombinu na kuweza kutekeleza shughuli zake vizuri kwa maendeleo ya nchi”, alieleza Dkt. Kazungu

Aidha Dkt. Kazungu, amekitaka Chuo hicho kujikita katika ubunifu kwa kubuni program mbalimbali za kitaaluma zitakazowavutia wanafunzi, jambo litakaosababisha ongezeko la wanafunzi na kuimarika kwa kipato cha Chuo, hivyo kupunguza utegemezi kwa Bajeti Kuu ya Serikali.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC), Dkt. Frank Mkumbo, alisema kuwa kuna utofauti kati ya takwimu rasmi zinazotolewa na chuo hicho na takwimu zinazotolewa na vyuo vingine, kwa kuwa EASTC hutoa takwimu rasmi za Serikali zikiwemo za mfumuko wa bei, idadi ya watu na hata kiwango cha uzalishaji wa bidhaa nchini.

Dkt. Mkumbo, ameahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Kazungu, yakiwemo ya kutoa mafunzo kwa maafisa mipango na kuanzisha kozi zitakazo ongeza idadi ya Wanafunzi lakini pia kuendelea kushirikiana na wizara katika kutekeleza shughuli mbalimbali.

Mkuu huyo wa Chuo amesema, ziara ya Naibu Katibu Mkuu Dkt. Kazungu, katika taasisi zilizopo chini ya Wizaya ya Fedha na Mipango, kikiwemo Chuo cha EASTC imekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa utaimarisha upatikanaji wa mapato na kuongeza ufanisi wa utoaji elimu.

Mwisho.


from MPEKUZI

Comments