Sakata La Kodi Ya Pango La Ardhi Lazidi Kuwa Chungu Kwa Baadhi Ya Kampuni Mwanza

Na Munir Shemweta, WANMM MWANZA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amezidi kuzibana Taasisi na Makampuni yenye madeni makubwa ya kodi ya pango la ardhi ambapo ametua mkoani Mwanza na kuyabana makampuni na taasisi nane ambazo kwa ujumla wake zinadaiwa zaidi ya milioni 900.

Kampuni na taasisi alizotembelea Dkt Mabula ni Synergy Tanzania Ltd, Ideal Development Ltd, Birchard Oil Ltd, Shule za Musabe, Taasisi ya Taifa ya Utafiti Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Ndamavyo Auto Spares, Jesse & Company Ltd na Maabara ya Taifa ya Udhibiti Samaki na Mazao ya Uvuvi.

Akizungumza katika ziara yake hiyo ya kufuatilia madeni ya kodi ya pango la ardhi mwishoni mwa wiki, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema ziara hiyo anayoifanya ya kuwafikia wale wenye madeni makubwa inafuatia baadhi ya kampuni na taasisi zinazodaiwa kushindwa kulipa ama kurekebisha madeni yao baada ya kikao cha Juni 11, 2019 kilichowakutanisha wadaiwa zaidi ya 200 jijini Dodoma

katika mwanzo wa ziara yake kwenye shule za Musabe, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi  alimueleza mmiliki wa shule hizo Daniel Musabe kulipa deni lake la kodi ya pango la ardhi linalofikia milioni 57.4 katika viwanja vyake vinne anavyomiliki kufikia tarehe 31 Julai 2019 ili kuepuka kufikishwa katika Baraza la Ardhi na Nyumba.

Hata hivyo, Mmiliki wa Shule hizo ambazo ni za Chekechea, Msingi na Sekondari alimueleza Dkt Mabula kuwa yuko tayari kulipa deni la kodi ya pango la ardhi lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na changamoto za kibiashara ambapo hata hivyo aliahidi kulipa kiasi anachodaiwa kuanzia Agosti 2019 na kumaliza deni lote ifikapo Desemba 2019.

Akiwa katika Kampuni ya Birchard Oil Limited, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Mabula ambaye aliambatana na Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizarani Denis Masami aliitaka kampuni hiyo kulipa kiasi inachodaiwa cha kodi ya pango la ardhi inayofikia milioni 85,235,050 ikiwa ni pamoja na malimbikizo ya kodi za miaka ya nyuma.

Meneja uhusiano wa Kampuni hiyo inayojishughulisha na uzalishaji Mafuta na Marobota ya Pamba Arshad Jetha alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi kuwa kampuni yake pamoja na kudaiwa kodi ya pango la ardhi kwa baadhi ya viwanja inavyomiliki lakini baadhi yake alishalipia hivyo aliomba kuhakikiwa madeni yake ili kupata deni halisi.

Ideal Development Ltd kupitia Meneja wake Burnanuddin Rajbhai alikiri deni la kodi ya pango la ardhi linalofikia milioni 79 na kuomba kupewa muda wa kulipa katika awamu tatu tofauti. Hata hivyo, Naibu Waziri wa Ardhi alizitaka kampuni na Taasisi zilizokubali kulipa madeni  kuandika barua ya kueleza namna zitakavyolipa na muda wa mwisho wa kulipa madeni yao katika ofisi za ardhi za halmashauri husika na nakala za barua hizo ziende ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi wa Kanda ya Ziwa.

Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwa Makwasa Biswalo aliionya kampuni ya Ideal Development Ltd kwa kushindwa kutekeleza makubaliano yaliyofikia ya kulipa deni lake na kuieleza kuwa hatua itakayofuata kwa kampuni hiyo ni kufikishwa katika Baraza la Ardhi na suala la kuingia makubaliano ya malipo haliwezi kufanyika kwa mara ya pili.

Kampuni ya Synergy Tanzania Ltd Kupitia kwa Meneja Utawala wake Florence Kivamba iliahidi kuandika barua ya makubaliano ya kulipa deni la milioni 43 inayodaiwa ingawa alioamba kufanya mawasiliano na uongozi wa juu kwa kuwa ziara ya Naibu Waziri wa Ardhi ilikuwa ya kushtukiza na uongozi haukuwepo.

Akiwa katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Mabula aliueleza uongozi wa Taasisi hiyo kuwa inadaiwa jumla ya shilingi milioni 515,713,900 ya kodi ya pango la ardhi na taasisi hiyo haijawahi kulipa kodi hiyo tangu mwaka 1996.

Mkurugenzi wa NIMR mkoa wa Mwanza Safari Kinuhi alijitetea kwa kueleza kuwa taasisi yake inapaswa kusamehewa kulipa kodi ya pango la ardhi kwa kuwa haiko kibiashara bali inatoa huduma kwa wananchi na kuboresha afya ingawa aliahidi kuwasiliana na uongozi wa juu kuhusiana na suala hilo.

Hata hivyo, Dkt Mabula alimueleza kuwa Taasisi yake inapaswa kufuata sheria wakati wa kuomba kusamehewa kodi ya pango la ardhi huku Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizarani Denis Masami akisisitiza kuwa hata kama Taasisi hiyo itasamehewa kulipa kodi hiyo lakini deni la nyuma lazima lilipwe kwa kuwa sheria ya msamaha itaanza pale tamko la msamaha lilipotoka.

Maabara ya Taifa ya Udhibiti Samaki na Mazao ya Uvuvi iliyopo eneo la Nyegezi ilionekana kutokuwa na hati ya eneo inalomiliki ingawa Afisa Mfawidhi wa Taasisi hiyo Emanuel Mundoko alijitetea kwa kueleza kuwa awali Taasisi hiyo ilikuwa sehemu ya chuo cha Uvuvi na sasa inajitegemea hivyo hawajui madeni halisi wanayodaiwa.


from MPEKUZI

Comments