Bilioni 14.9 yakusanywa na TRA Njombe

Na Amiri kilagalila-Njombe
Mamlaka ya mapato Tanzania TRA mkoa wa Njombe imefanikiwa kukusanya bilioni 14.9 ya mapato katika mwaka wa fedha 2018/2019 hadi sasa ,licha ya bajeti ya makadilio kuwa bil 17 na kutoa pongezi kwa wilaya ya njombe ambayo imekusanya zaidi ya asilimia 70.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa wiki ya elimu kwa mlipa kodi mkoani Njombe iliyofanyika mjini Makambako,Afisa mwandamizi wa kodi mkoa wa Njombe Adeliki Alphonce amesema kuwa licha ya kufanikiwa kukusanya kiasi hicho cha fedha lakini bado kuna upungufu wa shilingi bilioni 3.1 ili kukamilisha lengo.

"Mpaka sasa wananchi wenzangu tumeweza kukusanya shilingi bilioni 14.9 katika yale malengo ya bilioni 17 bado tunaupungufu wa bilioni 3.1 kwa hiyo wafanyabiashara tujitoe katika muda uliobaki tuweze kufikisha lengo,tuzitumie hizi mashine za elektroniki na tusione kama TRA wanakuja kutusumbua"alisema Adeliko Alphonce

Aidha katika kuhakikisha mkoa wa Njombe unakuwa kinara kwa ukusanyaji wa mapato mkuu wa wilaya ya Njombe akizindua wiki ya elimu kwa mlipa kodi amezitaka halmashauri kuondoa vikwazo visivyo na tija kwa wawekezaji wa viwanda ili kuwavutia wawekezaji na kukuza uchumi wa kaya , mkoa na taifa kwa ujumla.

"Kama alivyotueleza mh.Rais alipokuwa kwenye mkutano wake wa kwanza katika mkoa wa Njombe kwenye wilaya ya Njombe sehemu inaitwa Lwangu halmashauri ya mji wa Njombe alisema,tunatabia ya kuchelewesha wawekezaji na haya yanafanywa ndani ya halmashauri na mimi nirudie kuwaomba wale wanaohusika na ardhi saidieni ili tuhakikishe kwamba ili tuweze kulipa kodi na kwa ziada na sisi mchango wetu uonekane mkubwa zaidi tupate viwanda"alisema Msafiri 

Licha ya mamlaka hiyo kuonyesha juhudi katika kukusanya mapato lakini Wafanyabiashara mjini Makambako mkoani hapo ulipofanyika uzinduzi, wamesema kuwa hali ya biashara imezidi kuwa mbaya na kusababisha wafanyabiashara wenye mitaji midogo kufunga maduka kutokana na kuwepo kwa mrundikano mkubwa wa tozo ambapo wamedai kuwa wamekuwa wakitozwa tozo zaidi ya kumi katika mlango mmoja wa biashara hatua ambayo inakwamisha maendeleo yao na kuiomba serikali kuweka tozo hizo katika kapu moja.


from MPEKUZI

Comments