Upelelezi kesi ya Yusufali na wenzake wakamilika....February 21 Watasomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Februari 21, 2019 kumsomea maelezo ya mashahidi na vielelezo, mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Yusufali na wenzake wawili.

Mbali na Yusufali, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi Namba 8/2019 ni Arifal Paliwalla na Meneja wa Benki ya I&M tawi la  Kariakoo, Sameer Khan.

Yusufali maarufu kwa majina ya Choma, Mohamedali au Mohamed Jamalee na wenzake, wanakabiliwa na mashtaka 506 yakiwamo ya kutakatisha fedha, kukwepa kodi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh24 bilioni.

Uamuzi huo umetolewa jana Jumatatu Februari 18, 2019  na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya hakimu anayesikiliza shauri hilo kuwa na kazi nyingine.

Awali, Wakili kutoka Takukuru, Leonard Swai alidai mbele ya Hakimu Shaidi kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na hakimu anayesikiliza shauri hilo, Augustine Rwizile ana kazi nyingine, hivyo wanaomba ahirisho fupi kwa ajili ya kupanga tarehe ya kuwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo.

“Washtakiwa wote wapo mbele ya mahakama yako na kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya Mashahidi na vielelezo, washtakiwa hawa,” alidai Swai na kuongeza:

“Lakini hakimu anayesikiliza shauri hili ana kazi nyingine hivyo, tunaomba tarehe fupi kwa ajili ya kupangiwa tarehe ya kuwasomea maelezo  ya washtakiwa"

Swai amedai kuwa tayari Takukuru imeshafungua taarifa ya kesi hiyo Mahakama Kuu Kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu Mahakama ya Mafisadi.

Swai baada ya kueleza hayo, Wakili wa utetezi, Jamhuri Johnson akisaidiaa na Hassan Kiangio, walikubaliana na hoja za upande wa mashtaka na kuiomba mahakama hiyo ipange tarehe fupi.

Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 21, 2019 na washtakiwa wamerudishwa mahabusu kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana.

Hatua ya kuwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo, washtakiwa hao inatokana na upelelezi wa kesi hiyo kukamilika.

Hata hivyo, washtakiwa hao wakishasomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo, wataulizwa kama wana maoni yoyote na kama hawana, kesi hiyo itahamishwa kutoka katika Mahakama ya Kisutu na kwenda  katika mahakama ya Mafisadi kwa ajili ya kuanza kusikilizwa rasmi.


from MPEKUZI

Comments