Nape Aiomba Familia ya Ruge Iruhusu Watu wa Nje Wachangie Matibabu Yake

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye ameiomba familia ya mkurugenzi wa vipindi wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba kuruhusu watu wa nje kushiriki katika kuchangia gharama zake za matibabu.

Nape amesema hayo leo Jumatatu Februari 18, 2019 wakati akihojiwa na kipindi cha 360 kinachorushwa na Clouds TV.

Amesema mchango ambao ameutoa Ruge kwa jamii na kugusa maisha ya watu wengi, ni vema familia yake nje ya Mutahaba ikapata nafasi ya kushiriki kwenye kuwezesha gharama za matibabu.

“Ruge ni mtu ambaye ana moyo wa kusaidia wengine bila kujali nini kitatokea, anaweza kukesha kwa ajili ya jambo la mtu, tusiwanyime watu hiyo fursa, tuwaruhusu wafanye kila wanachoweza kama familia yake ya nje washiriki baraka ya kumuuguza,” amesema.

“Ruge ni wa kwetu sote amegusa watu wengi sana, katika hili njia nzuri ni muhimu kuungana kama familia ya Ruge nje ya Mutahaba na kuanzisha kampeni ya kusaidia gharama za matibabu tukizingatia muda aliokaa hospitali,” ameongeza.

Nape amesema, “Mimi ni mtaalamu wa propaganda, Ruge ni bingwa wa propaganda anaweza kukibeba kitu kidogo kikawa kikubwa.”

Mdogo wake Ruge, Mbaki Mutahaba amesema tatizo linalomsumbua kaka yake ni figo ila kwa sasa  anaendelea vizuri, ikilinganishwa na awali.

“Yupo kwenye rehab, sio ICU na akiendelea hivi asilimia kubwa ataweza kufika kwenye hali ambayo tulikuwa tunamfahamu. Tulimpeleka Afrika Kusini tukitegemea matibabu yangekuwa ya muda mfupi kumbe imekuwa tofauti na gharama zimekuwa kubwa kupita kiasi ila tunashukuru Mungu.”

Kuhusu suala la gharama, Mbaki amesema, “Hatuwezi kuficha gharama ni kubwa na ikitokea mtu ameguswa na hili anataka kutusaidia sisi kama familia tuko tayari, miezi minne imekatika sasa tangu aende kwenye matibabu Afrika kusini.”

Mbaki amesema wamekuwa wakipata pole na dua kutoka kwa watu mbalimbali akiwamo Rais, John Magufuli 

“Kama kuna watu tumewakwaza kwa kuwa kimya juu ya taarifa za Ruge tunaomba mtuwie radhi lakini sisi kama familia tulifanya alichokipenda yeye kwa kuwa siku zote mambo yake amekuwa akiweka private,” amesema


from MPEKUZI

Comments