Mahakama yasema sio kosa kuendesha ukiwa umekunywa pombe

Mahakama ya Kiambu nchini Kenya imetoa hukumu ya aina yake, ikieleza kuwa kuendesha gari ukiwa amekunywa pombe sio kosa  kama unaweza kukidhibiti vyema chombo hicho cha moto.

Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kiambu, Bryan Khaemba ametoa maelezo hayo katika hukumu iliyomuachia huru mshtakiwa wa kosa la kuendesha pikipiki akiwa amelewa pombe. 

Mahakama hiyo imeamua kuwa, ili mtuhumiwa awe na hatia, inapaswa muendesha mashtaka kutoa ushahidi usioacha shaka kuwa mtu huyo hakuwa na uwezo wa kudhibiti chombo hicho cha moto.

Katika maelezo ya kesi hiyo, muendesha mashtaka alieleza kuwa mshtakiwa aliyetajwa kwa jina la Mugo aliendesha pikipiki akiwa amelewa, Mei 23 mwaka 2018 na kwamba alishindwa kukidhibiti chombo hicho vizuri, katika eneo la Banana-Ruaka, Kiambu.

Askari polisi aliyetoa ushahidi katika kesi hiyo, aliiambia Mahakama kuwa mtuhumiwa aliwashinda nguvu yeye na askari wenzake wawili walipotaka kumkamata, hivyo walishindwa kumkamata wakati wa tukio na kisha kumtafuta baadaye.

Maelezo hayo ndiyo yaliyomuokoa mshtakiwa, kwani Mahakama iliamini mtu aliyewashinda watu watatu, hata kama alikuwa amekunywa pombe hawezi kushindwa kudhibiti mwendo wa pikipiki yake.

“Kuwashinda askari watatu…! Hicho sio kitendo ambacho kingetegemewa kufanywa na mtu ambaye mnadai alikuwa amelewa hadi kushindwa kuendesha vizuri au kudhibiti chombo chake,” alisema Hakimu.

Alieleza kuwa mshtakiwa hakuwa ameathiriwa kwa kiwango kilichotajwa na pombe, kwani ingekuwa hivyo angekamatwa kirahisi na askari hao watatu.

“Kwa maana hiyo, Mahakama imebaini kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuwasilisha ushahidi usioacha shaka wa namna ambavyo mtuhumiwa alishindwa kukidhibiti chombo cha moto alichokuwa akikiendesha,” Citizen inamkariri Hakimu Khaemba.

Mahakama hiyo iliweka msisitizo kuwa kuendesha ukiwa umekunywa pombe tu, haitoshi kuwa kosa kwa mujibu wa sheria za Kenya.


from MPEKUZI

Comments