Mahakama yakataa kupokea maelezo ya Onyo Kesi ya Malinzi na Wenzake

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imekataa kupokea maelezo ya onyo ya washtakiwa Flora Rauya na Miriam Zayumba yalihojiwa na ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa( Takukuru ),Frank Mkilanya kama kielelezo cha ushahidi katika kesi hiyo.

Hakimu Mkazi Maira Kasonde alikataa kupokea maelezo hayo leo kama kielelezo cha ushahidi katika kesi hiyo baada ya Mkilanya ambaye ni shahidi wa 11 wa upande wa mashtaka kuomba mahakamani hapo yapokelewe kama kielelezo cha ushahidi.

Akikataa kupokea maelezo hayo, Hakimu Maira alisema kutokana na kifungu cha 50 na 51(a) ambacho kinawapa uwezo polisi kuchukua maelezo onyo ya washtakiwa, kinawataka kuyachukua ndani ya saa nne tangu kukamatwa yawe yamekwisha chukuliwa.

Katika maelezo ya shahidi huyo wa 11 wa upande wa mashtaka yalionyesha muda wakuanza kuchukuliwa na mwisho wa kumaliza, lakini tatizo limejitokeza watuhumiwa walivyochukuliwa maelezo haijaelezwa walikamatwa wapi na lini.

Hivyo kwa kuwa ni suala la kisheria maelezo hayo hayawezi kupokelewa kwa sababu hayajakidhi vigezo.

Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo Hakimu Maira aliiahirisha kesi hiyo hadi Machi 5, mwaka huu ambapo wataendelea kusikiliza ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.

Mbali na washtakiwa hao, wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Malinzi, Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine(46) na Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga (27).

Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 30 katika kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha wa dola za Marekani 173,335.


from MPEKUZI

Comments