Mahakama ya Afrika Yaipa Serikali ya Tanzania Siku 45 za Kujitetea

Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCPHR), imetoa siku 45 kwa Serikali ya Tanzania, ikiitaka itoe utetezi kuhusu maombi yaliyofunguliwa mahakamani hapo kutaka matokeo ya uchaguzi ya Rais yapingwe mahakamani.

Kwa mujibu wa barua ya Msajili wa AfCPHR, Dk. Robert Eno, amri hiyo inafuatia ombi namba 018/2018 lililofunguliwa mahakamani hapo na mlalamikaji Jebra Kambole dhidi ya mlalamikiwa ambaye ni Serikali ya Tanzania.

Katika barua yake ya Februari 14, mwaka huu, yenye kumbukumbu namba AfCHPR/Reg./APPL/018/2018/008, Msajili Dk. Eno, amemtaka malalamikiwa kutoa utetezi wake ndani ya siku 45.

“Mlalamikiwa anajulishwa na mahakama hii, kwa mujibu wa maslahi ya haki, kuendelea na kutoa hukumu kwa mujibu wa maombi yaliyowasilishwa iwapo haitapokea utetezi wowote ndani ya siku 45 baada ya kupokea barua hii.

“Msajili anakutaarifu (mlalamikiwa) kwamba mlalamikaji ameomba kutolewa uamuzi kuhusu kushindwa kwako (mlalamikiwa), kutoa utetezi wa shauri alilofungua kwa mujibu wa kanuni 55(1) ya Kanuni za Mahakama hiyo.

“Pale ambao upande mmoja unashindwa kuonekana mahakamani au unashindwa kutetea kesi yake, mahakama inaweza kwa kuzingatia maombi yaliyowasilishwa na upande mwingine, kupitisha hukumu/uamuzi baada ya kujiridhisha kwamba upande ulioshindwa kufanya hivyo, ulipelekewa hati ya maombi ya shauri husika pamoja na nyaraka zake zote kwa ajili ya mwenendo wa shauri hilo,” ilisema sehemu ya barua hiyo.


from MPEKUZI

Comments