Kenya, Somalia Ndani ya Bifu Zito......Kenya yamrudisha nyumbani balozi wake wa Somalia huku ikimtimua yule wa Somalia nchini humo

Mgogoro kuhusu umiliki wa eneo la mpaka wa bahari Hindi kati ya Kenya na Somalia umeongezeka baada ya Kenya  kuamua kukata uhusiano wa kidiplomasia na Somalia kufuatia madai kwamba Somalia imenadi maeneo ya mafuta yaliopo mpakani.

Siku ya Jumamosi jioni , Kenya  ilitangaza kuwa inamrudisha nyumbani balozi wake aliyepo Mogadishu Luteni Jenerali mstaafu Lucas Tumbo , ikidai kuwa uamuzi wa Somalia kupiga mnada eneo moja la mafuta mjini London wiki iliopita ni sawa na uchokozi dhidi yake na mali yake asili.

Vilevile Nairobi ilimrudisha nyumbani balozi wa Somalia nchini Kenya Mohamed Nur na kuchochea zaidi kesi inayoendelea mjini The Hague kuwa mgogoro wa kisiasa kati ya Nairobi na Mogadishu.

''Uchokozi wa kiwango hiki hautakubaliwa na Wakenya wote, pamoja na watu wasamaria wema wanaoamini sheria ya kimataifa mbali na hatua za kusuluhisha migogoro'', katibu wa maswala ya kigeni nchini Kenya Macharia Kamau alisema.

''Kwa kupuuza suluhu ya sheria za kimataifa kuhusu mipaka ama makubaliano ya kisiasa kupitia diplomasia , serikali ya Somalia imeonyesha wazi bado haijakomaa kisiasa'' , aliongezea katibu huyo.

Katikati ya mgogoro huo ni eneo lililopo ndani ya bahari Hindi lenye ukubwa wa mraba maili 62,000 .

Haijulikani ni taifa gani linalomiliki eneo hilo lakini linaaminika kumiliki kiwango cha juu cha mafuta na gesi.
 
Kenya inasisitiza kwamba mpaka huo unakwenda sambamba na laini ya latitude na tayari ilikuwa imeuza leseni za uchimbaji mafuta kwa makampuni ya uchimbaji madini katika eneo hilo kabla ya mzozo huo kuchipuka.

Kenya sasa imedai kwamba uchimbaji wa mafuta katika eneo hilo umesimamishwa kwa muda kama ishara ya uhusiano mwema, lakini Somalia inasisitiza kuwa hiyo haitoshi.

Somalia vilevile inasisitiza kuwa mpaka wake unafaa kuwa sambamba na mpaka wake wa kusini.

Swala hilo liliwasilishwa katika mahakama ya kimataifa ya haki ICJ mnamo mwezi Aprili 2014 baada ya majadiliano kugonga mwamba.

Kenya ilikuwa imepoteza kesi hiyo hapo awali na kulazmika kuwasilisha kesi yenye uzito mkubwa.

Wataalam wa baharini hapo awali wameonya kwamba Kenya huenda ikapoteza kesi nzima iwapo uamuzi wa hapo awali utarudiwa.

Hatahivyo Kenya iliendelea na swala hilo huku aliyekuwa jaji mkuu Githu Muigai akiliwakilisha taifa hilo mbele ya mahakama ya mjini Hague.
 
Iwapo Kenya itapoteza kesi hiyo basi italazimika kuwachilia visima vyake vitatu kati ya 20 katika bahari hindi kwa Somalia.

Visima vinavyozozaniwa ni L-21, L-23 na L-24 . Swala nyeti la mgogoro huo kati ya Kenya na Somalia ni alama ya mpaka wa baharini.

Credit:BBC



from MPEKUZI

Comments