Bilioni 27.4 Zapitishwa Mpango Wa Bajeti 2019-2020 Halmashauri Ya Wilaya Ya Njombe

Na  Amiri kilagalila
Baraza la madiwani halmashauri ya wilaya ya Njombe mkoani Njombe limepitisha  mpango wa bajeti wa shiringi bilioni 27.4 kwa mwaka wa fedha 2019-2020 ukilinganisha na bajeti ya mwaka wa fedha 2018-2019 iliyokuwa shiringi bilioni 22.5  sawa na ongezeko la asilimia 18 ya bajeti hiyo.

Akisoma mpango wa bajeti hiyo kabla ya kupitishwa katika kikao cha baraza maalum la madiwani halmashauri ya wilaya ya Njombe,afisa mipango wa halmashauri hiyo ndugu Daniel Anganile,amesema ongezeko la asilimia 18 limetokana na kuongeza makisio ya vyanzo vya mapato ikiwa ni pamoja na bajeti ya mishahara ya watumishi.

“Katika mwaka wa fedha 2019-2020 halmashauri inategemea kukusanya kiasi hicho cha fedha ambayo kati ya fedha hiyo shiringi bilioni 20.7 ni ruzuku ya mishahara,sh.bilioni moja ni ruzuku ya matumizi mengineyo,shiringi bilioni 3.1 ni ruzuku ya miradi ya maendeleo,bilioni 1.9 ni fedha ya mapato ya ndani huku milioni 465 ni mapato maalum” amesema afisa mipango

 Mbunge wa jimbo la Lupembe Jorum hongoli ametoa ushauri kwa halmashauri kuangali miradi midogo kwa kila kata itakayoweza kuleta mapato kwa wakati kuliko kuangalia miradi mikubwa itakayochelewa kuleta matokeo chanya.

“Nimeona kuna mradi mkubwa kwenye taarifa wa kujenga mradi wa jengo la biashara utakaoleta fedha nyingi na halmashauri ikapata mapato ila mimi nilikuwa naomba wakati tunafikiri hayo basi tufikirie pia na miradi midogo katika kata zetu wataalamu wetu na madiwani tushirikiane huko kuna fursa ipi tunayoweza kuwekeza hata kama ni mradi mdogo lakini mwisho wa siku ukazalisha kitu fulani” Amesema mbunge Hongoli

Poul Kinyamagoha ni diwani wa kata ya Ninga na Isaya Myamba ni diwani wa kata ya Igongolo wamesema kuwa bajeti hiyo inagusa katika maeneo yote ya changamoto za wananchi ikiwemo maji na zahanati hivyo ushirikiano zaidi unahitajika katika ukusanyaji wa mapato.

Aidha mwenendo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani katika halmashauri ya wilaya ya Njombe katika kipindi cha nusu mwaka  uliopita,halmashauri imekwenda vizuri kwa kuwa mbele kwa asilimia 5 ya ukusanyaji kutokana na mikakati ya kudhibiti mianya ya utoroshaji wa mapato licha ya kuwepo kwa changamoto.


from MPEKUZI

Comments