Serikali Yapokea vifaa vya Dola za Marekani 30,000 kudhibiti uhamiaji haramu Nchini

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, amepokea vifaa vya kudhibiti uhamiaji haramu katika mipaka mbalimbali nchini vyenye thamani ya Dola za Marekani 30,000 (sawa na Sh. mil. 68.7)
 
Akizungumza na waandishi wa habari jana, wakati wa kupokea vifaa hivyo, Masauni alisema vifaa hivyo vitasaidia kwa kiwango kikubwa kudhibiti mipakani ambako hutumika kama mwanya wa kuingilia wahamiaji haramu na kwamba lengo ni kuhakikisha wanakomesha kabisa wahamiaji haramu ikiwamo vitendo vyote vya uhalifu katika mipaka ya nchi.

"Vifaa hivi ni kama sehemu ya kuongeza nguvu katika mipaka yetu ya nchi katika udhibiti wa wahamiaji haramu na vitendo vyote vya uhalifu katika mipaka yetu yote nchini," alisema Masauni na kuongeza:

"Tunataka kuhakikisha tunakomesha vitendo vyote katika mipaka yote, wahamiaji haramu, bidhaa haramu zinazopita katika mipaka yetu na mambo mengine yote."

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wahamiaji (IOM), Dk. Qasim Sufi, alisema wametoa vifaa hivyo kama mchango wao katika kupambana na vitendo vya uhamiaji haramu Tanzania.

Alisema wataendelea kusaidia katika nyanja hiyo, ili kuhakikisha tatizo hilo hasa katika sehemu za mipaka ya nchi linakomeshwa.

"Tunaamini kwamba kwa vifaa hivi kidogo tulivyotoa kwa Serikali ya Tanzania itasaidia kupambana na vitendo vya uhamiaji haramu kama siyo kumaliza kabisa tatizo hili, lakini tunaahidi kwamba kwa ushirikiano mzuri tulionao na nchi hii, tutaendelea kutoa mchango wetu pale tunapoweza," alisema Dk. Sufi.


from MPEKUZI

Comments