Kamati Yapendekeza Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi Waliyepigana Oifisi Waondolewe

Kamati iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira kuchunguza mgogoro wa kiuongozi wilayani Mwanga imependekeza mkuu wa wilaya hiyo (DC), Aaron Mbogho na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya (DED), Zefrin Lubuva waondolewe ama wote au mmoja wao.

Mghwira aliamua kuunda kamati hiyo kwenda kuchunguza mgogoro huo baada ya hivi karibuni Lubuva kudaiwa kupigana ofisini na ofisa mmoja wa wilaya hiyo, jambo lililozua sintofahamu ya kiuongozi wilayani humo.

Hatua ya viongozi hao wa Serikali kupigana ofisini ilielezwa kuwa ni baada ya mkurugenzi kutohudhuria kikao kimoja kilichokuwa kimepangwa kufanyika Januari 17, huku akituma mwakilishi.

Mghwira amesema wakurugenzi, wakuu wa wilaya pamoja na watendaji wengine wa Serikali mkoani humo wanapaswa kufanya kazi kwa kushirikiana na si kuendeleza migogoro ambayo haina tija.

Alisema mgogoro uliopo wilayani Mwanga na kitendo cha watendaji kupigana ofisini ni kufikia ukomo wa kufikiri na hakipaswi kufanywa na viongozi wa Serikali.

Alisema mawasiliano mazuri, uvumilivu na kuheshimiana kimamlaka ni jambo muhimu la kuzingatia kwani kutofanya hivyo kunachelewesha maendeleo ya wananchi.


from MPEKUZI

Comments