Jeshi la Polisi Lazungumzia Ma RPC Watatu Waliotumbuliwa na Waziri Lugola

Msemaji wa Jeshi la  polisi, DCP Ahmed Msangi, amesema suala la makamanda watatu wa polisi ambao Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, alitangaza kuwavua nyadhifa zao lipo mezani kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, likisubiri utatuzi.
 
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Msangi alisema kwa nafasi yake hawezi kulizungumzia suala hilo kwa kuwa tayari liko mezani kwa IGP ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kulizungumzia na kulisimamia.
 
“Mimi nikiwa msemaji wa polisi siwezi kulizungumzia suala hilo kwa kuwa liko mezani kwa IGP,” alisema alipoulizwa kuhusu utekelezaji wa agizo la Lugola.
 
Wiki iliyopita, Lugola alitangaza kutengua uteuzi wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Polisi Ilala, Salum Hamduni, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Emmanuel Lukula na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Ramadhani Ng’azi. 

Licha ya agizo hilo la Lugola, makamanda hao waliendela kubaki ofisini.
 
Siku chache baadaye Lugola alipoulizwa juu ya agizo lake kutotekelezwa, alisema: “Sina taarifa kwamba agizo langu halijatekelezwa, lakini nilimpa IGP muda wa utekelezaji, kwa hiyo naamini litatekelezwa. Saa nyingine watu hawajui kutengua mtu ni mamlaka, na mimi ninayo. Utekelezaji unaendelea.” 


from MPEKUZI

Comments