Stendi Mpya ya Mabasi ya Mikoani Dar Hatarini Kuota Mbawa.....Waziri Atoa Siku 6

Waziri  wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo ametoa siku sita  kupata taarifa ya kina kuhusu mradi wa kituo cha mabasi cha Mbezi Luis.

Jafo aliyasema hayo jana akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa ofisi yake Magogoni Jijini Dar es Salaam na kudai kuwa iwapo hatopata maelezo ya kina, basi fedha za mradi huo zitapelekwa kwenye halmashauri nyingine ili zifanye shuguli nyingine za maendeleo.

Alisema mradi huo wa kituo cha mabasi cha Mbezi Luis umetengewa fedha nyingi ambayo ni Sh bilioni 50.9 lakini anashangazwa hadi sasa unasuasua.

“Seriakali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 105 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali 67 za Wilaya na shilingi bilioni 50.9 za ujenzi wa kituo cha mabasi cha Mbezi Luis.

“Dar es Salaam ni mkoa ambao umenufaika zaidi na fedha za mradi lakini mpaka sasa inasikitisha kituo cha mabasi cha Mbezi Luis kinasuausa.

Awali mradi huo ulipangwa kuanza Julai mwaka 2017 lakini mpaka sasa haujaanza kitendo ambacho kimemlazimu Waziri Jafo kutoa siku sita kwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam kumpa maelezo ya kina ya ujenzi wa kituo hicho.

“Ukiachia machinjio ya kisasa Vingunguti,  ujenzi wa soko la Kisutu, soko la Mburahati, soko la Magomeni kuna mradi mkubwa wa  Stendi ya Mabasi ya Mbezi Luisi.

“Bahati mbaya nimetoa maelekezo katika vipindi mbali mbali miradi hii itekelezwe ndani ya muda, lakini nasikitika hatujaridhishwa na spidi ya mradi wa mabasi ya Mbezi Luisi na una fedha nyingi zaidi.

“Natoa maelekezo mpaka Jumatano wiki ijayo tarehe 19, nipate taarifa ya mwenendo wa mradi wamefikia wapi na mkandarasi anaanza vipi kazi, na kama maelekezo haya nikiona yanasuasua, tutaziondoa fedha hizo za mradi na  kupeleka kwenye Halmashauri nyingine, hii naweka wazi.


from MPEKUZI

Comments