Rais wa Uganda, Yoweri Museven Agoma Kuachia Madaraka

Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, amewaambia wazi wapinzani wake kuwa hana mpango wa kuachia madaraka hivi karibuni, hivyo waachane na mawazo yao ya kuwaza kiti hicho.

Rais Museveni ameyasema hayo kwenye mkutano wa ndani wa chama ambao uliwakusanya pamoja viongozi wa vyama vilivyopo Bungeni, mkutano uliofanyika Jijini Kampala.

Museveni amesema amefurahia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea kwenye mkutano huo, ambapo aliwaambia wapinzani wake kwamba hatofikiria kubadilishana madaraka mpaka pale atakaporidhishwa na Ustawi na usalama wa kimkakati wa nchi za Afrika.

“Nasikia watu kama Mao wanazungumzia kuachia madaraka, ni kwa namna gani watakaa kwenye umati na kumuona Museveni akikabidhi madaraka. Hicho ndicho kitu muhimu kwake. Sidhani kama ni sahihi kwa yeye kusema hivyo, badala ya kuzungumzia hatma ya Afrika, mnaongelea vitu visivyo na maana, uchaguzi, nani atakuwa nani. Na ndio kwa sababu nilisema kama bado nina nguvu nitaendelea”, amesema Rais Museveni katika mkutanoni huo.

Rais Museveni aliendelea kusema kwamba, ”huo ndio mtazamo wangu, sitastaafu pale ambapo masuala ya muhimu ya Afrika ambayo inakaribia kuangamia hayajajadiliwa, na nyinyi mnajadili vitu vidogo, uchaguzi, mtakaowachagua, mnawachagua wafanye nini haswa!?, hilo ndilo mnalotakiwa kujibu”.

Museveni ambaye anakaribia kutimiza miaka 33 akiwa madarakani, alitamka hayo yote baada ya kauli ya Kiongozi wa chama cha kidemokrasia, Jenerali Norbet Mao, ambaye alisema ana ndoto ya siku kumuona Rais Museveni akikabidhi madaraka kwa mtu mwingine kwenye viwanja vya Kololo, jambo ambalo aliwakatisha matumaini kabisa wapinzani wake.

Ikumbukwe hivi karibuni Uganda wamabadilisha katiba yao na kuondoa ukomo wa umri wa kugombea Urais, kitu mbacho kitamruhusu Rais Museveni kuendelea kugombea tena na kuendelea kuwa Rais wa Uganda iwapo atashinda.


from MPEKUZI

Comments