Nape Apinga Mfumo wa Serikali Kuhusu Malipo ya Korosho kwa Wakulima

Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye ameibuka na kuwatetea wakulima baada ya serikali kutangaza hivi karibuni kuanza kutowalipa pesa wakulima wanaomiliki korosho walizozipata kwa kuzinunua kutoka kwa wenzao kwa mfumo wa 'kangomba' pasipo kuwa na mashamba.

Nape amesema kuwa mfumo huo unaoendelea sasa unawapa mateso wakulima na kupendekeza kuwa ili kumaliza tatizo hilo, ni vyema serikali kuviwezesha vyama vya ushirika kupitia Benki ya Maendeleo ya Wakulima (TADB) kulipa sehemu ya malipo kwa wakulima hao mara tu korosho inapofika ghalani.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Nape Nnauye ameandika, "dawa ya kangomba ni kubadili mfumo wa malipo ya korosho kwa wakulima, kwa kuviwezesha Vyama vya Ushirika kupitia TADB kulipa sehemu ya malipo mara tu korosho inapofika ghalani. Hiki kinachoendelea sasa hakiwezi kumaliza kangomba, ni mateso tu kwa wakulima!,"

Rais Magufuli wakati akitangaza uamuzi wa serikali kununua korosho za wakulima, Novemba 13 Jijini Dar es salaam alisema kuwa serikali itanunua korosho zote za wakulima kwa bei ya sh 3,300 kwa kilo baada ya wanunuzi binafsi kushindwa kutimiza matakwa ya serikali.

Hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Rukia Muwango alisema kuwa wakulima wote waliouza zao hilo bila kuwa na mashamba, wajiandae kisaikolojia kwani hawatolipwa mpaka watakapoonesha mashamba waliyovuna korosho hizo.


from MPEKUZI

Comments