Marekani Yachukizwa Na Kitendo Cha Urusi Kutuma Ndege Hatari Za Kuangusha Mabomu Venezuela

Maafisa wakuu wa Urusi na Marekani wamejibizana baada ya ndege mbili kubwa za kuangusha mabomu za Urusi kutua nchini Venezuela, taifa linalopatikana Amerika Kusini.

Ndege hizo mbili zina uwezo wa kubeba silaha za nyuklia.

Ndege hizo za kivita aina ya Tu-160 zilitua Venezuela Jumattau katika kile kinachoonekana kama jaribio la kuonyesha uungaji mkono wa Urusi kwa rais wa Kisoshialisti wa Venezuela Nicolás Maduro ambaye amekuwa akikabiliwa na shinikizo.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amesema kitendo hicho ni sawa na "serikali mbili fisadi kufuja mali ya umma."

Serikali ya Urusi imesema maneno yake hayo "hayafai hata kidogo."
 
Ndege hizo mbili za kivita zenye uwezo wa kusafiri mwendo mrefu bila kutua zilitua katika uwanja wa ndege wa Simón Bolívar viungani mwa mji mkuu wa Venezuela, Caracas, zikiandamana na ndege nyingine mbili za Urusi.

Venezuela na Urusi zimekuwa marafiki kwa muda mrefu na ndege hizo mbili za kivita ziliwahi kutumwa tena taifa hilo mwaka 2008, zikiwa pamoja na manowari moja yenye uwezo wa kurusha makombora. Ndege hizo zilifika tena Venezuela mwaka 2013.

Kitendo cha sasa kimetokea siku chache tu baada ya rais Maduro kukutana na Rais Vladimir Putin mjini Moscow.

Waziri wa Ulinzi wa Venezuela Vladimir Padrino alisema ndege hizo ni sehemu ya mazoezi ya pamoja ya kijeshi kati ya Venezuela na mshirika wake Urusi.

"Hili tunalifanya kwa pamoja na marafiki zetu, kwa sababu tuna marafiki duniani ambao hutetea na kuheshimu uhusiano wa usawa."
 
"Tunajiandaa kuilinda Venezuela hadi hatua ya mwisho ikilazimu," alisema waziri huyo akionekana kurejelea tuhuma za mara kwa mara ambazo zimekuwa zikitolewa na serikali ya nchi hiyo kwamba yapo mataifa yanayotaka kupindua serikali ya nchi hiyo.
 
Rais Maduro alisema Jumapili kwamba kuna juhudi zinazoendelea kwa sasa "zikiratibiwa moja kwa moja kutoka White House (Marekani) za kuvuruga maisha ya kidemokrasia Venezuela na kutekeleza mapinduzi dhidi ya serikali iliyochaguliwa kikatiba, kidemokrasia na iliyo huru ya taifa letu."

Bw Pompeo alishutumu kitendo cha kutumwa kwa ndege hizo za Urusi kwenye Twitter.
 
Msemaji wa Rais wa Urusi Vladimir Putin, Dmitry Peskov, amesema tamko la Pompeo si la kidiplomasia hata kidogo.


from MPEKUZI

Comments