Bunge Umoja wa Ulaya Latoa Tamko Kuhusu Matukio ya Utekaji na Hali ya Siasa Tanzania

Bunge la Umoja wa Ulaya (EU) limetaja mambo kadhaa ikiwamo kuandamwa kwa wanasiasa wa upinzani nchini Tanzania na kueleza kuwa, yanafanyika kinyume na maazimio ambayo nchi hiyo imeridhia.

Mambo mengine yaliyoelezwa na Bunge hilo ni kufungiwa kwa baadhi ya redio binafsi na magazeti, kukamatwa kwa waandishi wa habari.

Katika azimio namba 2018/2969 lililopitishwa katika kikao chake mjini Brussels, Ubelgiji Bunge hilo limesema halifurahishwi na hali inavyoendelea Tanzania.

Azimio hilo ambalo limesambazwa maeneo mbalimbali linaeleza kuwa katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko la matukio yanayoashiria hali ya ukandamizaji wa haki za binadamu na limeitaka Serikali ya Tanzania kutupia macho maeneo hayo.

Maeneo mengine ambayo Bunge hilo limebainisha ni matukio kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa, sheria inayohusu makosa ya mtandao na ushoga.

Limetaka uchunguzi huru kuhusiana na matukio ya kushambuliwa na kukamatwa kwa waandishi wa habari, watetezi wa haki za binadamu na wanachama wa vyama vya siasa na kusisitiza wale watakaokuwa nyuma ya vitendo hivyo kuchukuliwa hatua.



from MPEKUZI

Comments