Viongozi Watiwa Mbaroni kwa kutafuna fedha za maji

Jeshi la Polisi Wilayani Muheza, limewatia mbaroni watu watatu kwa amri ya Mkuu wa Wilaya, Mwanasha Tumbo, baada ya kutuhumiwa na wananchi wametafuna fedha za serikali.

Watu hao ambao ni wajumbe wa kamati ya maji, walitiwa mbaroni juzi katika mkutano wa hadhara uliyofanyika katika kijiji cha Ubembe, kata ya Nkumba wilayani Muheza. Walituhumiwa kuwa wametafuna fedha za bodi ya maji ya kata hiyo.

Waliokumbwa na kadhia hiyo ni Mwenyekiti wa Bodi ya maji ya Kata, Athuman Mhando, katibu wake Martin John na mhasibu wake aliyefahamika kwa jina moja la Semgalawe.

Akizungumza katika mkutano huo, Athumani Salehe alisema viongozi hao hawajawahi hata siku moja kuwasomea mapato na matumiziyanayotokana na mradi wa maji.

Salehe alisema kutokana na tuhuma hizo, walifika wakaguzi wa ndani wa hesabu wa wilaya na kubainika kwamba viongozi hao  wametafuna fedha hizo ambazo zilitokana na malipo ya maji ya kila mwezi.

Alisema walipofika wakaguzi hao ilionekana kuna dosari kubwa katika matumizi ya fedha hizo na kwamba walitakiwa wachukuliwe hatua lakini mpaka siku ya mkutano walikuwa bado. Hatua hiyo pia ilisababisha wananchi kugoma kulipa fedha za maji.

Kutokana na maelezo hayo, Tumbo aliagiza kukamatwa viongozi hao na kupelekwa polisi kuhojiwa kuhusiana natuhuma hizo kabla ya kufikishwa mahakamani.

Katika hatua nyingine, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nkumba, Bruno Mayenja, amekamatwa na polisi wilayani hapa kwa amri ya mkuu wa wilaya, kwa madai ya kufanya ubadhirifu wa fedha za serikali katika matukio tofauti kwenye maeneo alikokuwa akifanya kazi.

Mayenja alikamatwa baada ya kudaiwa kutafuna Sh. milioni 2.7 za mauzo ya shamba la Hassan Rashid, mkazi wa kijiji cha Masimbani kwa ajili ya kumlipa deni Demi Limo kwa amri ya mahakama lakin hakuzifikisha kwa mhusika.



from MPEKUZI

Comments