Mwita Waitara Alivyojibu Maswali Bungeni Kwa Mara ya Kwanza

Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mwita Waitara amejibu swali kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe na Rais Dkt, John Pombe Magufuli kushika nafasi hiyo.

Katika mkutano huo wa Bunge, Mwita Waitara aliulizwa swali na Mbunge wa Hannang Mary Nagu,  ambaye alihoji ni lini serikali itaunga mkono juhudi za wananchi katika kujenga mabweni kwa wafugaji wa wilaya hiyo.

Akijibu swali hilo Waitara amesema “serikali inatambua uwepo wa mabweni kwa maeneo ya wafugaji, ndiyo maana tumepeleka zaidi ya bilioni 1 kwa ajili ya kuboresha elimu, na serikali itaendelea kutoa kipaumbele ili kutoa haki kwa watoto wa wafugaji kusoma.”

“Lakini pia nimuombe mheshimiwa Mbunge, kwa kuwa ndiyo nimeanza kazi nimuombe Mbunge asubirie nitafanya ziara jimboni kwake ili tuweze kufahamu namna ya kusaidia wanafunzi.”

Mbali na Mbunge huyo pia Naibu Waziri huyo alijibu maswali ya wabunge wengine wa chama chake akiwemo Pauline Gekul na James Ole Milya.

Waitara ni miongoni mwa wabunge ambao walihamia Chama Cha Mapinduzi na kufanikiwa kugombea tena nafasi yake ya ubunge kwenye jimbo la Ukonga ambapo aliapishwa bungeni Novemba 6 mwaka huu na Novemba 10 Rais Magufuli alimteua kushika nafasi hiyo.


from MPEKUZI

Comments