Mbunge wa CCM, Maulid Mtulia Ataka Fidia Kwa Polisi Wanaofariki Wakiwa Kazini Iongezwe Hadi Milioni 50

Mbunge wa Kinondoni (CCM) Maulid Mtulia ameitaka Serikali kuongeza kiwango cha fidia kwa polisi wanaofariki wakiwa kazini kutoka Sh15 milioni hadi Sh50 milioni ili kiende na wakati.

Akiuliza swali la nyongeza bungeni leo Novemba 14 2018, Mtulia amesema kiasi cha fidia kinachotolewa hakilingani na hali ya sasa na kwamba polisi wamekuwa wakifanya kazi kubwa.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amesema wazo hilo ni zuri na kwamba Serikali imelichukulia na italifanyia kazi.

Katika swali la msingi, Mtulia amesema kazi wanayoifanya polisi ni ngumu na hatari hasa kwa kuzingatia matukio ya mauaji ya askari yanyoongezeka

“Serikali ina mpango gani wa kuongezea posho ya mazingira magumu na hasa baada ya askari wetu kulengwa wao binafsi kinyume na ilivyokuwa awali?”amehoji.

Akijibu swali hilo Lugola amesema askari anapopoteza maisha akiwa kazini hulipwa fidia ya Sh 15milioni.

Amesema anapojeruhiwa na kupata ulemavu wa kudumu wakati akitekeleza wajibu wake, Serikali hulipa fidia kulingana na madhara aliyoyapata baada ya kuthibitishwa na Kamati ya Maslahi kwa askari walioumia kazini ambayo inajumuisha daktari.

“Kwa sasa Serikali haina mpango wa kuongeza posho ya mazingira magumu kwa askari polisi hata hivyo Serikali inakusudia kuhuhisha posho mbalimbali za askari ili ziweze kulipwa kulingana na mazingira halisi ya sasa,”amesema.


from MPEKUZI

Comments