Vigogo ACACIA Wafikishwa Mahakamani Wakikabiliwa na Mashitaka 39

Aliyekuwa makamu wa rais wa kampuni ya Acacia, Deo Mwanyika na Alex Lugendo ambaye ni mshauri wa Serikali ndani ya kampuni hiyo, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashtaka 39, yakiwemo ya utakatishaji fedha, kughushi na kula njama.

Washtakiwa wamesomewa mashtaka yao leo mbele ya Hakimu  Mkazi  Mfawidhi,  Kevin Mhina na Jopo la mawakili watatu waliokuwa wakiongozwa na wakili  wa  serikali  Mkuu,  Faraja  Nchimbi  akisaidiana na Wakili wa serikali Mwandamizi,  Shadrack  Kimaro na Jackilline Nyantori.

Mbali na Mwanyika na Lugendo, washtakiwa wengine ni kampuni ya Mgodi ya Pangea, North Mara, Exploration na Bulyanhulu.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama 3, mashtaka yakughushi 7. Utakatishaji wa fedha 17, Kuwasilisha nyaraka  za uongo  kwa  Mamlaka ya Mapato Tanzanian (TRA), shtaka moja, kuongoza uhalifu wa kupangwa shtaka moja, kukwepa kodi, mashtaka 8 na shtaka moja la kutoa Rushwa.
 
Akisoma hati ya mashtaka wakili Nchimbi amedai washtakiwa hao pamoja na watu wengine ambao bado hawajakamatwa, walitenda makosa hayo kati ya Aprili 11.2008 na June 30.2007 katika sehemu tofauti za jiji la dar es Salaam, Kahama Mkoani Shinyanga, Tarime Mara, Biharamulo Kagera maeneo ambayo yapo katika Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo katika mji wa Johannesburg, Afrika Kusini, Toronto Canada na nchini  Uingereza.

Imedaiwa katika kipindi hicho na mahali huko washtakiwa hao kwa pamoja wakiwa na watu wengine ambao bado hawajakamatwa walikula njama ya ya kutenda makosa ya kughushi na ukwepaji wa Kodi.

Pia mshtakiwa Mwanyika (56), na Lugendo (46), wanadaiwa kutoa msaada katika kusimamia mkakati wa kihalifu kwa nia ya kupata faida.

 Aidha washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Mei 16.2008 na Desemba 31,2008 huko Kahama na Biaramulo, walitoa tamko la uongo kwa kamishna Generali wa TRA kwa nia ya kukwepa kodi kulipa USD 9,309,600 ambayo ilikuwa ni kodi iliyopaswa kulipwa kwa TRA.

Katika mashtaka ya utakatishaji, washtakiwa Mwanyika na Lugendo wanadaiwa kati ya Desemba 2009 na Desemba 31 2018 katika maeneo tofauti ndani na nje ya nchi ya Tanzania kwa pamoja na wengine ambao hawapo mahakamani, walisaidia mgodi wa North Mara kuhamisha fedha kiasi cha USD 374,243,943,45 huku wakijua kuwa fedha hizo ni zao la makosa ya kughushi na kukwepa kodi.

Pia washtakiwa wanadaiwa kati ya Novemba 2. 2012 na Novemba 27. 2015 huko Shinyanga walitoa Rushwa ya sh. 718,520,001.76 kwa Hussein Kashindye ambaye  ni mkuu wa upelelezi makosa ya jinai wa Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kumshawishi ili aweze kuachana na uchunguzi wa makosa ya jinai yaliyokuwa yametendwa na Mgodi wa Bulyanhulu.

Katika shtaka la kughushi washtakiwa hao wakiwa na nia ya ulaghai waligushi mkataba wa mkopo wakitaka kuonyesha kwamba Aprili 30.2014 Kampuni ya Pangea limited ilikubali kukopa USD 90,000,000 ikiwa na riba Kutoka benki ya kimataifa ya barrick huku wakijua kuwa siyo kweli.

Katika shtaka la kutoa nyaraka ya uongo, mshtakiwa Mwanyika anadaiwa Aprili 30.2018 huko BOT iliyopo wilaya ya ilala, kwa makusudi aliwasilisha  nyaraka ya uongo ya mkopo baina ya kampuni mgodi wa Bulyanhulu na Barrick international bank Corp kwa madhumuni ya kuonesha kuwa, kati ya June 2001 na Desemba 13.2007 Bulyanhulu walijipatia mkopo usio na faida wa USD 416,100,000 kutoka Barrick.

 Hata hivyo wa washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika. Na kesi itatajwa tena Oktoba 31, mwaka huu.



from MPEKUZI

Comments