Tanzania yajipanga kuteka soko la muhogo China

Serikali  imewataka wazalishaji wa zao la muhogo nchini kuongeza uzalishaji ili kuwawezesha kupata soko la uhakika nchini China.

Hatua hiyo itaifanya Tanzania kuongeza wigo wa kusafirisha zao hilo nchini humo ambapo kwa mwaka 2017 inakadiriwa kupeleka bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani laki tatu sawa na Sh.milioni 687, huku China ikiingiza bidhaa zake hapa nchini zenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 3.1.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Profesa Siza Tumbo katika mkutano wa wadau wa wa zao la Muhogo kitaifa ambao umeandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania(TARI), Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Kitropiki(IITA) na Wizara ya Kilimo, kitengo cha Mpango wa Maendeleo ya sekta ya kilimo awamu ya pili(ASDP II).

Mkutano huo unalenga kuandaa mipango ya kuendeleza zao hilo kuwa kibiashara na kuchangia katika maendeleo ya nchi.

Alisema kama Taifa kunatakiwa kuwapo na msimamo wa kuchangamkia soko la zao hilo nchini China kutokana na fursa ya kibiashara iliyopo.

“Uzalishaji upo chini kitakwimu lakini kuuhalisia haipo hivyo, sasa tunatakiwa tuwe ma champion kwenye uzalishaji wa zao hili ni zuri sana ili tuweze kuleta mageuzi kwenye zao hili,”alisema.

Alibainisha kuwa zao hilo nchini ni la pili kwa umuhimu zaidi katika mazao ya chakula baada ya mahindi na asilimia 84 ya jumla ya uzalishaji nchini ni kwa matumizi ya chakula cha binadamu, lakini uzalishaji huo bado uko chini na zao hilo halijatumika kikamilifu.

Aidha aliwataka Watanzania kula vyakula vya asili ili kulinda afya zao kwa kuwa kumekuwapo na mtazamo hasi kwa jamii kuwa kuna baadhi ya mazao ikiwamo muhogo na mtama kwamba hayafai kwa chakula jambo ambalo ni upotoshaji.

Aliwataka wakulima wa muhogo kutokatishwa tamaa na kauli hizo badala yake waongeze nguvu katika uzalishaji ili waweze kushindana na masoko makubwa ikiwamo nchi ya China.

Tanzania ni nchi ya 12 kwenye uzalishaji mkubwa wa muhogo duniani na ya sita barani Afrika baada ya Nigeria, Kongo DRC, Ghana, Angola na Msumbiji ambapo kila mwaka unachangia asilimia 5.5 ya jumla ya uzalishaji wake duniani na asilimia 14 kwa Afrika.

Mahitaji ya baadaye ya zao la muhogo nchini Tanzania unalengwa kuongezeka na kuwa kati ya tani 530,000 na 630,000 na kwamba hali hiyo inatokana na kuongeza thamani ya muhogo kwa kutengenezea unga, wanga na kuwa malighafi katika viwanda vya bia, pipi na vitafunio, viwanda vya nguo, karatasi, rangi na dawa.



from MPEKUZI

Comments