Sakata la Mo Dewji Kutekwa: Watu 19 Akiwemo Haji Manara Waachiwa kwa Dhamana.

Watu 19 kati ya 26 waliokuwa wakishikiliwa na Polisi kufuatia tukio la kutekwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ wameachiwa kwa dhamana jana usiku Oktoba 15, 2018 akiwemo Afisa Habari wa Simba, Haji Manara.
 
Akithibitisha kuachiwa kwa watu hao leo Jumanne, Oktoba 16,  Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Lazaro Mambosasa amesema kufuatia kuachiwa kwa watu hao, polisi inaendelea kuwashikilia wengine saba ili kuendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Manara alishikiliwa na Jeshi la Polisi tangu 12, Oktoba kwa kosa la kusambaza taarifa hizo kwenye mitandao ya kijamii kwa madai ya kutumwa na familia jambo ambalo polisi imesema si za kweli.

Mapema Oktoba 11, baada ya kuenea kwa taarifa za kutekwa kwa mfanyabiashara huyo, Manara alisema kuwa taarifa hiyo ilimshtua kila mmoja na kwamba bado wanawaachia mamlaka husika kufanya kazi yake kumpata mwekezaji wao.

“Wanasimba wawe watulivu wakiliachia Jeshi la Polisi kufanya kazi yake na tunaamini MO atapatikana akiwa hai,” alisema Manara.

Mpaka jana Oktoba 15, walikuwa wameshikiliwa watu 26 kwa mujibu wa Kamanda Mambosasa, ambapo baadaye mchana familia ya mfanyabishara hiyo ilizungumza na vyombo vya habari na kutangaza dau la shilingi bilioni moja kwa mtu yeyote atayefanikisha kupatikana kwa Mohammed Dewji 'Mo Dewji'.


from MPEKUZI

Comments