Hatima ya Kubenea, Komu kujulikana leo

Hatima ya Mbunge wa Ubungo Saed Kubenia na yule wa Moshi vijini, Anthony Komu, itajulikana leo baada ya kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Jana, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kutangaza kikao hicho.

Alisema kitafanyika Dar es Salaam leo na ajenda kuu ni masuala yanayoendelea ndani na nje ya Chama hicho.

“Tutatoa taarifa rasmi juu ya maazimio ya kikao hiki kitakapomalizika,”  ilisema taarifa ya Mrema.

Taarifa hiyo imetolewa  siku chache baada ya sauti zinazoaminika kuwa ni za Kubenea na Komu, kusambaa kwenye mitandao ya jamii wakijadili kuwashughulikia baadhi ya viongozi wa chama hicho.

Kwa mujibu wa sauti hizo, Kubenea na Komu walikuwa wakipanga kumshughulikia Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob.

Awali inasikika sauti ikisema; “Boni hana msaada wowote kwenye haya mambo”.

Kisha inasikika sauti nyingine ikisema; “Anao msaada mkubwa sana kwa sababu Boni…ujue ndiyo wamemsambaratisha Waitara.

“Boni ni mjumbe wa kamati kuu, ni msema ovyo, ni mtu ambaye ana misimamo ya vuguvugu lakini anaheshimika.

“Kuna watu wanamchukulia kama ni mpiganaji, ni mtu mwenye msimamo ambao ndiyo hao wanampa uhalali Mbowe. Ukimuondoa Boni umempiga sana Mbowe, sana yaani.

“Unajua viko vitu vya msingi vya kufanya, ku – deal na Mbowe ni kwenye mambo ambayo ni halali”.

Hata hivyo baadhi ya watu wa karibu na Komu walidai   mbunge huyo alituma kwa makosa sauti hiyo katika kundi la WhatsApp la Kaskazini bila kujua.

Hata hivyo wabunge hao walipoulizwa walikana kuhusika na sauti hizo na kudai kuwa zimetengenezwa kwa lengo la kuwachafua.


from MPEKUZI

Comments